DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha warsha ya tatu kwa wadau wa sekta ya fedha kuhusu masuala ya usalama wa Mifumo ya Tehama na Mitandao ya Mawasiliano kwa Timu ya Mwitikio wa Kukabili Majanga ya Kompyuta ya Sekta ya Fedha (TZ-FINCERT).


Jukumu la timu hiyo ni kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika sekta hiyo ili kuwawezesha watambue na wakabiliane na matukio ya usalama wa mifumo ya TEHAMA.
Akifungua warsha hiyo iliyofanyika katika Ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam, tarehe 20 Novemba, 2024, Naibu Gavana wa BoT (Utawala na Udhbiti wa Ndani), Bw. Julian Banzi Raphael, amesema warsha hii inalenga kuweka taratibu za kuripoti na kushirikishana taarifa za kiintelijensia za usalama wa mifumo ya TEHAMA miongoni mwa wadau wa TZ-FinCERT.
Ameeleza kuwa maendeleo ya kidijitali katika sekta ya fedha yameleta changamoto mbalimbali hususani katika usalama wa mifumo ya TEHAMA.
“Katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na maendeleo hayo na kutambua umuhimu wa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, Benki Kuu imeanzisha TZ-FinCERT kwa mujibu wa sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta yaani Electronic and Postal Communications Act (EPOCA) ya mwaka 2010.”


Wataalam hao ni pamoja na wawakilishi kutoka taasisi 49, kati ya hizo 37 zikiwa za watoa Huduma za Kifedha zisizo Benki na zilizobaki 12 zikiwa ni taasisi za Serikali.