NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, hadi kufikia Novemba 12,2024 imetoa leseni 2,200 kwa watoa huduma ndogo za fedha daraja la pili.
Meneja Msaidizi Idara ya Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Mary Ngasa ameyasema hayo leo Novemba 14,2024 katika semina kwa wahariri na waandishi wa habari.
Semina hiyo ambayo inafanyika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam inaangazia usimamizi wa mikopo ya mitandaoni.
"Benki Kuu inaendelea kupokea maombi na kutoa leseni za watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili.
"Hadi kufikia Novemba 12,2024 zaidi ya maombi 2,872 yalipokelewa na kati ya hayo, taasisi 2,200 zimepatiwa leseni."
Pia, amesema Benki Kuu inaendelea kuhuisha na kuchapisha orodha ya watoa huduma ndogo za fedha daraja la pili waliosajiliwa na kupewa leseni na Benki Kuu.
"Orodha hii inaonesha jina la taasisi, mahali ilipo, namba ya leseni, tarehe ya leseni,wamiliki na namba za mawasiliano."
Ngasa amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, Benki Kuu ya Tanzania imepewa jukumu la kusajili (kutoa leseni), kudhibiti na kusimamia taasisi za huduma ndogo za fedha nchini.
Amesema,sheria hiyo imegawa watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja manne.
Daraja la kwanza linaundwa na taasisi za kibenki zinazotoa huduma ndogo za fedha (Microfinance Banks).
Pia, daraja la pili amesema, linaundwa na watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana (non deposit taking Microfinance Service Provider).
Daraja la tatu amesema, linaundwa na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) ambapo limekasimiwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC).
Kwa upande wa daraja la nne,amesema linaundwa na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha (community microfinance group).
Amesema, daraja hilo la nne limekasimiwa kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).