MWANZA-Waandishi wa habari wametakiwa kuelewa vizuri uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuondoa noti za zamani katika mzunguko ili waweze kuwaelimisha vizuri wananchi tayari kwa utekelezaji wa mpango huo kuanzia Januari 2025.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mwanza, Bi. Gloria Mwaikambo, wakati akifungua semina ya siku mbili ya waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa inayofanyika tawini hapo.
Amesema, katika semina hiyo wataelezwa sababu za uamuzi wa kuondoa fedha za zamani katika mzunguko, ili wakielewa wawe mabalozi wazuri kupitia vyombo vyao vya habari kuwaeleza wananchi.
Pamoja na mada hiyo, washiriki wa semina hiyo wapatao 36 kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Simiyu, Shinyanga na Kagera, watapata mawasilisho kuhusu majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania na uamuzi wa Benki Kuu kuanza kuandaa na kutekeleza sera ya fedha kwa kutumia Riba ya Benki Kuu.
Mada nyingine zitahusu kujua alama za usalama za fedha zetu, uamuzi wa Benki Kuu kununua dhahabu ili kukuza akiba yake ya fedha za kigeni na utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha-mafanikio na changamoto.
Akizungumza baada wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa Semina hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mwanza, Bw. Edwin Soko, ameishukuru Benki Kuu kwa kuandaa semina hii na kuahidi kwamba wataitumia ili kuboresha uandishi wao kuhusu masuala ya sekta ya fedha nchini.
“Kwa kuelewa kuhusu majukumu ya Benki Kuu, umuhimu wa kuhifadhi dhahabu kama sehemu ya fedha za kigeni na masuala ya mikopo, ikiwemo mikopo umiza, waandishi wa habari wataongeza uwezo wa kuandika vizuri zaidi habari ya uchumi fedha na biashara,” amesema Bw. Soko.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa semina ameiomba Benki Kuu kufikiria kutoa motisha kwa waandishi wa habari wanaoandika vizuri habari za uchumi. Tuzo hii itaongeza hamasa kwao kutumika vizuri zaidi."
Awali, Meneja Msaidizi kutoka Idara ya Mawasiliano, Bi. Noves Moses, alieleza kuwa kwa zaidi ya miaka 12 Benki Kuu imekuwa ikifanya semina kama hizi sehemu mbalimbali hapa nchini.