DODOMA-Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, amewaongoza watumishi wa Hospitali hii ya Rufaa ya Kanda ya Kati na waombolezaji wengine kumuaga mtumishi, Dkt George Dilunga, aliyefariki Novemba 19,2024 asubuhi.Dkt.Dilunga amefariki akiwa anapatiwa matibabu BMH. Alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura ya BMH.
Akiongea wakati wa ibada ya kuaga mwili wa marehemu, Mkurugenzi Mtendaji, Prof Abel Abel Makubi, ameshukuru kwa utumishi wake na kutaka watumishi wengine kuiga mfano.
"Alikuwa ni Daktari aliyeipenda kazi yake, muda wote alifatilia maendeleo ya wagonjwa kule idarani kwake. Hivyo ni alama aliyotuachia, ambayo tutaienzi," amesema Prof Makubi,wakati wa ibada ya kuaga mwili iliyofanyika BMH.
Wakimuelezea watumishi wenzake, Ndugu Paschal wa Idara ya Dharura BMH, amesema alikuwa mtu mwenye bidii sana kwenye taaluma yake, alikuwa mkufunzi wa timu za magonjwa ya dharura katika Hospitali na mikoa mbalimbali.
Naye Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Shakiru, amemualezea Dkt Dilunga kuwa alikuwa Daktari na mwanataaluma mahiri, ambapo alikuwa mwenyekiti wa Jopo la Kuandaa Mtaala wa Kozi ya Huduma za Afya za dharura UDOM.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Nelson Bukulu, amesema uongozi wa Mkoa umesikitishwa sana na kifo cha Dkt Dilunga kwani alikuwa na mchango mkubwa katika masuala ya dharura za kiafya katika mkoa na amewakilisha katika majanga mbalimbali likiwemo maporoko ya udongo Hanang, Manyara.