NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema, ndani ya mwezi Novemba,2024 pekee imekamata tani zaidi ya 2.2 za dawa za kulevya katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 25,2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
"Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imekamata jumla ya kilogramu 2,207.56 za dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam."
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, watuhumiwa saba wanashikiliwa kuhusiana na dawa hizo.
Amesema, kati ya dawa hizo zilizokamatwa Skanka ni kilogramu 1,500.6, Methamphetamine kilogramu 687.76, herion kilogramu 19.20 na chupa 10 za dawa za kulevya aina ya Fentanyl.
"Novemba 14,2024 jijini Dar es Salaam katika Wilaya ya Kigamboni, Mtaa wa Nyangwale watuhumiwa Mohamed Suleiman Bakar mwenye umri wa miaka 40 na Sullesh Said Mhailoh mwenye umri wa miaka 36 wote wakazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam walikamatwa wakiwa na kilogramu 1,350.4 za dawa za kulevya aina ya Skanka."
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba aliyopanga mtuhumumiwa Mohamed ambayo aliitumia kama ghala la kuhifadhi dawa hizo.
Pia, amesema dawa nyingine zilipatikana ndani ya gari aina ya Nissan Juke yenye namba za usajili T 534 EJC zikiwa tayari kwa kusambazwa.
"Tarehe hiyo hiyo, katika Mtaa wa Pweza Sinza E Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, mtuhumumiwa Iddy Mohamed Iddy mwenye umri wa miaka 46 mkazi wa Chanika Buyuni alikamatwa akiwa na kilogramu 150.6 za Skanka."
Amesema, dawa hizo zilikuwa zimefichwa kwenye boksi lililotengenezwa kwa bati gumu na kupachikwa kwenye chassis ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika Kusini LN87XJGP ambalo limekuwa likitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, Novemba 17,2024 katika Jiji la Tanga watuhumiwa Ally Kassim Ally mwenye umri wa miaka 52 na Fadhadi Ally Kassim mwenye umri wa miaka 36 walikamatwa Mtaa wa Mwakibila wakiwa na kilogramu 706.96 za dawa aina ya Heroin na Methamphetamine.
"Baadhi ya dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 714 EGX huku nyingine zikibainika kufichwa kwenye nyumba aliyopanga mtuhumumiwa."
Mbali na hayo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, Novemba 19,2024 katika Mtaa wa Kipata na Nyamwezi huko Kariakoo jijini Dar es Salaam watuhumiwa Michael Dona Mziwanda mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Tabata Segerea.
Sambamba na Tumpale Bernard Mwasakila mwenye umri wa miaka 32 mkazi wa Temeke Mikoroshini walikamatwa wakiwa na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl wakiwa nazo katika duka la Mpesa.
Katika operesheni hiyo, Kamishina Jenerali Lyimo amesema,wanashikilia magari matatu na boti moja ambazo zilihusika na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Amesema, wamebaini wahusika wa dawa za kulevya wamekuwa wakipanga nyumba na kuzigeuza kuwa maghala ya dawa za kulevya.
Ameeleza kuwa, mmiliki wa nyumba akibaini kosa linatendeka katika nyumba yake ana wajibu wa kutoa taarifa kwa mamlaka.
Vilevile amesema, mamlaka ina kanzi data ya wauzaji wa dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.
Hivyo, kupitia operesheni yao wanaendelea kumchomoa mmoja baada ya mwingine ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema, baada ya wauzaji wa dawa za kulevya jijini Dar es Salaam kubaini mbinu zao zimefichuka wameamua kuanza kushushia dawa hizo mkoani Tanga.
Pia, amesema wengi wanaofanya biashara ya dawa za kulevya wanawatumia waganga wa kienyeji wakiamini kuwa watawapa kinga.
Amesema, kuanzia sasa wote watakaokamatwa huku wakiwa na viashiria vya imani za kishirikina wataongozana na maafisa wa mamlaka hadi kwa waganga wao.
"Watambue kuwa Serikali huwa hailogwi. Serikali inafanya kazi zake kwa weledi na mbinu mbalimbali."
Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya watakuwa wanawakamata.
Tags
Breaking News
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
ZDCEA