NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata kinara wa dawa za kulevya jijini Dodoma, Suleiman Mbaruku Suleiman maarufu Nyanda mwenye umri wa miaka 52 ambaye mamlaka hiyo ilikuwa inamfuatilia kwa karibu kwa muda mrefu.
Nyanda alikuwa na mwenzake Kimwaga Msobi Lazaro mwenye umri wa miaka 37 ambapo hatua za kisheria dhidi yao zinaendelea.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Novemba 12,2024 ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
"Huyu Nyanda ni maarufu sana katika lile Jiji la Dodoma na waraibu ambao tunawatibu katika kituo pale Dodoma wengi wameharibiwa na huyu Nyanda.
"Mtuhumiwa Nyanda ni kinara wa biashara ya kulevya mkoani Dodoma ambaye tulikuwa tunamfuatilia kwa muda mrefu hadi tumemkamata.
Amesema wakazi hao wa Mtaa wa Kinyali uliopo Kata ya Viwanjani jijini humo walikutwa wakiwa na jumla ya gramu 392 za dawa za kulevya aina ya Heroin.
Wakati huo huo amesema,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024 na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya.
Sambamba na mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya huku watuhumiwa 58 wakikamatwa katika operesheni hizo.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kati ya dawa hizo kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba jijini Dar es Salaam zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
“Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inavyosababisha madhara kiafya, vile vile hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka na mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa na magonjwa haya wamelogwa."
Amesema,katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema,dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika.
“Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya.”
Pia,amesema kumekuwa na ongezeko la watumiaji wakubwa wa dawa za kulevya aina ya skanka ikiwa wanaoongoza ni wanawake, huku sababu ya ongezeko hilo ikitajwa kuwa ni kupambana na msongo wa mawazo ambao umekuwa ukiwasumbua hasa ukitokana na udanganyifu wanaokutana nao kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Pia, amesema licha ya mbinu nyingi kutumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya ili kuingiza dawa za kulevya nchini ikiwemo kutoa rushwa, mamlaka imejipanga kuhakikisha kila mbinu inadhibitiwa.
Amesema, mamlaka imekuja na mkakati kabambe wa kuhakikisha mizigo yote inayoingia nchini kupitia mipakani inakaguliwa kwa kutumia scanner maalum na pale ambapo kuna mizigo itapita ikiwa na dawa za kulevya, Afisa aliyehusika na ukaguzi atawajibishwa mara moja.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)