Diva na Niffer waandika barua kuomba msamaha kwa kuchangisha michango ajali ya ghorofa Kariakoo

DAR-Mtangazaji wa Wasafi FM, Diva Gissele Malinzi na mfanyabiashara, Jenifer Jovin Bilikwija (Niffer) wameandika barua za kuomba radhi baada ya kupatikana na tuhuma za kuchangisha michango kwa ajili ya waathirika wa ajali ya ghorofa Kariakoo bila
kufuata utaratibu wa Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wawili hao walikamatwa na Jeshi La Polisi kwa ajili ya mahojiano na waliendelea kubaki mahabusu wakisubiria kupatiwa dhamana.

Wawili hao baada ya kutambua makosa yao wameandika jumbe za kuomba radhi na kuomba kusamehewa kwa sababu walifanya hayo kwa kutokufahamu utaratibu huku wakiahidi kutorudia tena na kuwa mabalozi wema katika jamii.

Barua ya Jenifer Jovin Bilikwija
Barua ya Diva Gissele Malinzi
Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne Muliro alisema wanamshikilia na kuwahoji, Diva Gissele Malinzi (36) mkazi wa Mikocheni na Jenifer Jovin Bilikwija 25.

Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda Muliro alisema, "Novemba 16, 2024 eneo la Kariakoo Dar es salaam kulitokea tukio la kuporomoka kwa jengo la biashara,

“Wakati jitihada mbalimbali zikifanywa na Serikali na sekta binafsi kuhusiana na jinsi ya kuwaokoa watu katika eneo hilo, zilipatikana taarifa za watu wasio na mamlaka yoyote ya kisheria ya kushughulikia majanga yenye sura ya kitaifa, kuanza kukusanya pesa kwa kutumia akaunti zao binafsi suala ambalo ni kinyume na Sheria na Kanuni zinazoshughulikia majanga."

“Watuhumiwa wawili wamekamatwa na wanahojiwa kwa kina, waliokamatwa ni Diva Gissele Malinzi miaka 36, mkazi wa Mikocheni amekamatwa Dar es Salaam na Jenifer Jovin Bilikwija miaka 25, mkazi wa Salasala Kinondoni ambaye amekamatwa Dodoma na kurejeshwa Dar es salaam."

Kamanda Muliro alisema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam litashirikiana na mamlaka zingine za kisheria kuona hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa hawa.

Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa tahadhari na halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu au watu ambao yanapotokea matatizo au majanga wao huona ni fursa ya kujinufaisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news