DODOMA-Mbunge wa Jimbo la Kigamboni mkoani Dar es Salaam na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile amefariki.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb).
Ameeleza kuwa, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile amefariki usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulle.
"Kwa niaba ya Wabunge natoa pole kwa familia, wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi,"amesema Spika.
Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia inaendelea kuratibu shughuli za mazishi na taarifa zaidi zitaendelela kutolewa.