NDANI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jahazi limezidi kuzama.Hii ni kutokana na namna ambavyo, viongozi wa juu wa chama hicho wameendelea kusigana wenyewe kwa wenyewe huku wakiwekeana uzibe ili siri za yanayotendeka ndani zisitoke.
Sintofahamu iliyopo kati ya Mwenyekiti wa chama Taifa, Freeman Mbowe na Makamu wake, Tundu Lissu inaendelea kuibua maswali ambayo si tu kwamba hayana majibu kwa viongozi wenzao bali hata kwa wanachama.
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA na mgombea urais kupitia chama hicho, Dkt.Willbroad Slaa ni miongoni mwa wanachama wa chama hicho ambaye naye amekuwa na maswali lukuki kuhusu yanayoendelea ndani ya chama kupitia viongozi hao.
Kupitia uchambuzi wake Dkt.Slaa kuhusu tuhuma za Mbowe kuzuia mkutano wa Lissu huko wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro hivi karibuni, anaonekana ana maswali mengi kuhusu msuguano na kuwekeana uzibe kwa wawili hao ingawa kuyapata majibu ya moja kwa moja ni vigumu.
“Lissu anatazamwa kwa sura gani baada ya kutangaza lile suala la fedha, maana yake yote haya unaweza kuyajua.
“Hakuna mtu anayezungumzia, lakini alipotamka tunajua ilienda kwenye kamati kuu (CHADEMA), lakini hakuna taarifa iliyotoka nje na kwa maana hiyo, hatujui kama CHADEMA kama taasisi sasa imekubaliana na hayo yaliyotajwa na wamepokea kweli hizo hela.
“Hakuna namna jamii itajua kama wao hawatoki nje, kama wao hawatoki nje, hawatupi maazimio ya kamati kuu, yote mawili kama halmashauri yao, baada ya kamati kuu ilipelekewa wala sina hakika hata kama ilipelekewa.
“Msimamo ulikuwa nini, na kamati kuu kama haikupelekewa, Je? Kama hayo yamo mbona haikuchukua hatua kwa wahusika, lakini siyo tu mbona haikuchukua hatua, kama hakuna mbona haikusafisha chama.
"Kwa hiyo, kitendo kwamba chama hakikujisafisha au kuchukua jukumu la kujisafisha kitaondoaje hisia kwenye akili yetu,”amefafanua Dkt.Slaa kupitia uchambuzi wake kuhusu tuhuma za Mbowe kuzuia mkutano wa Lissu huko Same.
Mbowe na Lissu katika miaka ya karibuni wamekuwa na mgogoro mkubwa ndani ya CHADEMA ambao umegusa maeneo mbalimbali kuanzia upande wa itikadi, kisiasa, kiutawala na demokrasia ndani ya chama.
Ikumbukwe kuwa, Tundu Lissu ambaye alikuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA mwaka 2020 alikosoa utendaji wa Mbowe na baadhi ya viongozi wa chama kwa kushindwa kuweka mfumo mzuri wa uongozi hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu huo.
Aidha,Lissu alidai kuwa chama kilijikuta katika hali ya kutokuwa na mwelekeo kutokana na mgawanyiko wa kiutawala na ukosefu wa mkakati madhubuti wa kukabiliana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Vilevile,baada ya kurejea nchini kutoka uhamishoni nchini Ubelgiji, Lissu alionesha nia ya kutaka kugombea nafasi ya mwenyekiti wa chama, akidai kuwa chama kinahitaji mabadiliko ili kurudi kwenye ufanisi.
Uamuzi huo, ulitafsiriwa kama changamoto kwa Mbowe, ambaye alikuwa amekiongoza CHADEMA kwa kipindi kirefu na aliishiwa na nguvu za kisiasa na ushawishi wa ndani ya chama.
Ingawa, Mbowe alikataa wazo la kumwachia Lissu nafasi hiyo huku hali ya mgawanyiko ikiendelea kushamiri zaidi.
Tags
Habari