Dr.Manguruwe mahakamani akikabiliwa na mashtaka 28 ikiwemo utakatishaji wa fedha

DAR-Simon Mkondya maarufu kama Dr. Manguruwe (40) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka 28 ikiwemo utakatishaji wa fedha wa shilingi milioni 90.
Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Vanilla International Ltd amefikishwa mahakamani na mwenzake Rweymamu John (59) ambaye ni mkaguzi wa kampuni hiyo.

Wawili hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Dr.Manguruwe na mwenzake wanadaiwa walitenda makosa hayo tarehe tofauti kati ya Januari Mosi mwaka 2020 na Disemba Mosi mwaka 2023 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo ilidaiwa kwamba, mashtaka 19 ni ya kufanya biashara ya upatu ambapo katika kipindi hicho Mkondya akiwa kama Mkurugenzi na John akiwa kama mfanyakazi wa kampuni hiyo walifanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kupata faida mara mbili hadi tatu kulingana ya kiasi cha fedha watakazotoa.

Aidha,ilidaiwa kwamba, washtakiwa hao walijipatia kiasi cha shillingi milioni 92.2 kutoka kwa watu 19 tofauti.

Watu hao walitoa kiasi tofauti cha fedha ambapo aliwaahidi watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Iliendelea kudaiwa kwamba, mashtaka tisa ni ya utakatishaji yanayomkabili mshitakiwa Mkondya pekee ambapo kati ya Januari Mosi mwaka 2020 na Desemba Mosi 2023, akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya upatu.

Hata hivyo,baada ya kusomwa mashtaka hayo, Wakili Mrema alidai kutokana na mashtaka yanayowakabili, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza hivyo washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.

Wawili hao wamekosa dhamana kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokuwa na mamlaka ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 19,2024 huku washtakiwa wakipelekwa mahabusu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news