TANGA-Naibu Katibu Mkuu - Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Suleiman Serera, ameitaka Bodi ya Mkonge kufanya utafiti wa masoko kwa ngazi ya kimataifa ili kujua hali ya bei ya Mkonge ikilinganishwa na hapa nchini. Ameyasema hayo Novemba 18, 2024 wakati alipofanya kikao na Viongozi wa Bodi ya Mkonge na Wadau wa Kilimo hicho kilichofanyika jijini Tanga.
"Tujifunze kwa nchi za wenzetu, tuone ni kwa namna gani wanavyoweza kufanya uzalishaji na kujua ni viwanda vya aina gani tunatakiwa kuwa navyo kwakuwa kupitia kujifunza ndipo tunakoweza kupata fursa na mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya masoko ya zao la mkonge," amesema Dkt. Serera.
Aidha, Dkt. Serera ameitaka Bodi ya Mkonge kutafuta fursa ya uzalishaji wa mkonge katika mikoa mingine ili kuongeza uzalishaji na kukuza pato la taifa.
Naibu Katibu Mkuu - Kilimo ametoa rai kwa Wakulima wa zao la Mkonge kujifunza na kuona faida za Ushirika kwa kujiunga na AMCOS ambazo zinawasaidia wakulima kuwa pamoja na hata kujiunga na SACCOS ambazo ni suluhisho la mtaji.