NA DIRAMAKINI
WATU kadhaa wamehofiwa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa baada ya jengo la ghorofa nne kuanguka katika Mtaa wa Mchikichi na Manyema uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea leo Novemba 16,2024 ambapo Jeshi la zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wakiwemo wananchi wanaendelea na uokoaji.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam,Jumanne Murilo amewaomba wananchi wote waliopanda katika majengo ya jirani kushuka na kuacha kupiga picha za eneo hilo kwani kuwa karibu na jengo hilo ni hatari.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amewataka wananchi wote katika eneo la Kariakoo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo juhudi za uokoaji zinaendelea.
Chalamila amesema kuwa, jengo hilo lina maduka na stoo za kuhifadhia bidhaa, ambapo mpaka sasa wameokoa badhi ya majeruhi wa tukio hilo na kuwapaleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Amesema,wataendelea kutoa taarifa ya kiwango gani cha majeruhi ama vifo kutokana na ajali hiyo kadri watakavyopata.
"Niwaombe wafanyabiashara, marafiki zao na wote ambao wapo katika eneo hili tuendelee kuwa na subira, kwani tumefanya jitihada za kuleta mitambo ya uokoaji.
”Mnafahamu greda au skaveta haliwezi kupita barabarani mpaka libebwe na gari maalumu la kubeba mitambo, na kwa muda huu lipo karibu na hapa kuja kufanya maokozi.
"Niwatoe watu wote wasiwasi kuwa polisi kazi yao ni kulinda amani katika maeneo haya, ku-rescue ni kazi inayofanywa na kikosi maalumu."
Pia, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kwa watu wote ambao wamepatwa na janga hilo kwa kuharibikiwa au kupotea kwa mizigo yao, kujeruhiwa kwa ndugu zao, jamaa au rafiki zao na hata mwenye jengo husika.