NA MARY GWERA
Mahakama Nairobi
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Majaji Wakuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika leo tarehe 04 Novemba, 2024 wameungana na Jaji Mkuu wa Kenya ambaye pia ni Rais wa Mahakama ya Juu ya Nchi hiyo, Mhe. Martha Koome pamoja na watumishi wa Mahakama nchini humo kushiriki katika ufunguzi wa mkutano wa sherehe za maadhimisho ya miaka 12 ya Mahakama ya Juu ya Kenya tangu kuanzishwa kwake.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt.William Samoei Ruto (kulia) akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) wakati wa sherehe za ufunguzi wa mkutano wa kuadhimisha miaka 12 ya Mahakama ya Juu ya Kenya leo tarehe 04 Novemba, 2024 katika eneo la Mahakama ya Juu Kenya. Katikati ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Mhe. Martha Koome.
Mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria wa ndani na nje ya nchi hiyo umefunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt.William Samoei Ruto ambaye katika hotuba yake ameipongeza Mahakama ya Juu Kenya kwa kusimamia Katiba katika kipindi chote cha miaka 12.
“Mahakama imesimama kama mlinzi mwaminifu wa Katiba yetu, mtetezi wa haki za kimsingi na nguzo ya demokrasia. Uwezo wake endelevu wa kutatua masuala tata ya kikatiba bado ni muhimu kwa uhai wa kitaasisi wa taifa letu,” amesema Mhe. Dkt. Ruto.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt.William Samoei Ruto (wa pili kulia) akiwa katika ufunguzi wa sherehe za kuadhimisha miaka 12 ya Mahakama ya Juu ya Kenya iliyofanyika leo tarehe 04 Novemba, 2024 jijini Nairobi. Kulia kwake ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Mhe. Martha Koome.
Rais Ruto amesema, Mfumo wa kazi ambao Mahakama ya Juu imeunda katika kipindi cha miaka 12 ni mpana na una mamlaka, na kwamba Mahakama hiyo imeonesha uwezo wake wa kushughulikia masuala tata, kufafanua sheria, kuleta utulivu wa sera na kuafiki matarajio ya watu wa Kenya.
Mhe. Dkt. Ruto ametoa rai kwa Mahakama hiyo kuendelea kutoa haki na kuwa Mahakama inayotekeleza wajibu wake ipasavyo kama ambavyo imekuwa ikitoa katika kipindi chote cha miaka 12 ya kuanzishwa kwake.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt.William Samoei Ruto akifungua mkutano wa sherehe za maadhimisho ya miaka 12 ya Mahakama ya Juu Kenya leo tarehe 04 Novemba, 2024 jijini Nairobi.
Rais Ruto ameongeza kuwa, ili kuthamini mafanikio yanayowakilishwa na uundwaji wa Mahakama ya Juu, ni lazima turudie masomo magumu ya mgogoro wa uchaguzi wa urais wa 2007 ambapo ameeleza kwamba, mgogoro huo ulifichua kushindwa kabisa kwa utaratibu na mmomonyoko mkubwa wa imani ya umma katika michakato ya uchaguzi na Mahakama, na hivyo kuvunja imani ya watu katika utawala wa sheria.
Alisema, matokeo ya uchaguzi yenye utata yalizua migogoro ambayo ilikaribia kulipeleka taifa kwenye ukingo wa kuporomoka kidemokrasia.
Katika hatua nyingine, Rais huyo ameipongeza Mahakama ya Juu ya Mahakama kwa kupiga hatua katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuiomba Mahakama hiyo kuisaidia Mihimili mingine ya Dola katika nchi hiyo kutumia TEHAMA ili kusaidia kuleta maendeleo hususani katika kukuza mapato ya nchi hiyo.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Mhe. Martha Koome akitoa hotuba yake wakati wa sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 12 ya Mahakama ya Juu Kenya.
Naye, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Mhe. Martha Koome akitoa hotuba katika mkutano huo, amesema katika kipindi cha miaka kumi na miwili iliyopita, Mahakama ya Juu imekuwa na jukumu la kuleta mabadiliko, kuchagiza sheria za Kenya na maendeleo ya kijamii na kisiasa ya nchi.
“Kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu kama mfasiri na mlezi mkuu wa Katiba, kunajumuisha matarajio kwamba Mahakama ya Juu inatoa uhakika na kutabirika katika kusuluhisha mizozo isiyoepukika inayotokea ndani ya jamii yetu. Kwa hiyo, tunathibitisha wazo kwamba mustakabali wetu upo katika kujenga taasisi imara na imara, ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo ya taifa,” amesema Mhe. Koome.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa katika ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 12 ya Mahakama ya Juu ya Kenya. Kushoto ni Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Mhe. Nestor Kayobera.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa, licha ya mitego isiyoepukika, mamlaka ya Mahakama imetumia Katiba kimakusudi kama chombo chenye nguvu cha kuendeleza ustawi wa watu binafsi na kuendesha mabadiliko ya jamii kwa manufaa ya wote.
Amesema, Maamuzi ya Mahakama pia yameshughulikia moja kwa moja masuala ya haki za ardhi, haki za binadamu, kijamii na haki ya kiuchumi, na sheria ya familia.
Jaji wa Mahakama ya Juu Kenya, Mhe. Njoki Ndung'u akizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 12 ya Mahakama ya Juu Kenya.
Ametoa rai kwa Serikali na wadau kutumia njia mbadala usuluhishi (ADR) katika utatuzi wa migogoro mbalimbali ili kuokoa muda ambao utatumika katika shughuli za maendeleo.
Mkutano huo uliofunguliwa leo unakuwa ni mwanzo wa maadhimisho hayo ambayo yatahitimishwa tarehe 06 Novemba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt.William Samoei Ruto (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki waliohudhuria katika sherehe hizo leo tarehe 04 Novemba, 2024.(Picha na MARY GWERA, Mahakama ya Tanzania).
Katika kipindi hicho kutakuwa na mijadala mbalimbali kuhusu Mahakama hiyo yote ikilenga kuboresha zaidi utoaji huduma ya haki.