Jaji Mkuu wa Tanzania atoa wito kwa washiriki CJCA kutoa maamuzi yanayozingatia haki na utu

NA MARY GWERA
Mahakama Zimbabwe

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Majaji wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) kutafakari kama uamuzi wanaotoa unazingatia haki na utu wa binadamu kama inavyoeleza kaulimbiu ya mkutano wa saba wa Mahakama hizo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa mada kuhusu 'Dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba' jana tarehe 31 Oktoba, 2024 kwa washiriki wa Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) unaofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Akizungumza Oktoba 31, 2024 wakati akiwasilisha mada kuhusu Dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba kwa washiriki wa Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) unaofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa, utu wa binadamu ni suala muhimu la kuzingatia katika kila eneo.

“Naomba sote tujiulize, je maamuzi tunayotoa yanaakisi utu na haki za binadamu? suala hili ni muhimu kuniuliza kwa kuwa utu wa binadamu ni muhimu kuuzingatia na kutekeleza,” alisema Jaji Mkuu wa Tanzania.

Alieleza kuwa, Tanzania inazingatia utu na haki za binadamu ambapo aliainisha kuwa Ibara ya 12 (2) ya Katiba ya Tanzania inaeleza kuwa, “Kila mtu anastahiki kutambuliwa na kuheshimiwa utu wake.”
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba' jana tarehe 31 Oktoba, 2024 mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Aliongeza kuwa, Mahakama ya Tanzania inazingatia pia haki na utu wa binadamu katika utoaji wa maamuzi yake ambapo alitoa mifano ya baadhi ya mashauri hayo.

Katika wasilisho lake, Mhe. Prof. Juma alitoa mifano kadhaa inayozungumzia maana ya utu wa binadamu ambapo pia alimnukuhu Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati akipigania uhuru.

Alimnukuhu akisema, “tumeshakubaliana katika misingi fulani; sasa ni wakati wa kuweka kanuni hizi katika utendaji. Wakati wote ambao TANU imekuwa ikimpigia debe Uhuru tumeegemeza mapambano yetu juu ya imani yetu ya usawa na utu wa wanadamu wote na juu ya Tamko la Haki za Binadamu,” (J.K. Nyerere: Ujumbe wa uhuru kwa TANU kama ulivyochapishwa na Gazeti la Uhuru).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa pamoja na wazungumzaji wenzake ambao kwa pamoja walishiriki katika paneli ya kuzungumzia mada ya 'Dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba' waliowasilisha katika Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) unaofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Kadhalika, akiwasilisha mada hiyo, Mhe. Prof. Juma alitoa tafsiri kadhaa za neno ‘Utu wa Binadamu’ huku akirejea maana kutoka kwa waandishi mbalimbali, ambapo tafsiri mojawapo inaeleza dhana ya utu wa binadamu ni imani kwamba watu wote wana thamani maalum ambayo inahusishwa pekee na ubinadamu wao na haina uhusiano wowote na tabaka lao, rangi, jinsia, dini, uwezo au sababu nyingine yoyote isipokuwa wao kuwa binadamu.

Aliongeza kwa kuelezea, utu wa binadamu huku akimnukuhu moja ya kitabu kilichoandikwa na Aharon Baraka, (“Wajibu wa Utu wa Binadamu kama Thamani ya Kikatiba,” iliyochapishwa mtandaoni na Chuo Kikuu cha Cambridge Press 05 Februari 2015].

Alieleza kwamba, Mwandishi huyo alizingatia maadili matatu ya utu wa binadamu kuwa, moja ni tunu ya kikatiba inayounganisha haki za binadamu kuwa kitu kimoja, mbili ni kanuni ya kifasiri ya kuamua upeo wa haki za kikatiba, ikiwa ni pamoja na haki ya utu wa binadamu na tatu ni muhimu katika kutathmini uwiano wa sheria inayozuia haki ya kikatiba.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akiwa katika Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) unaofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe. Kushoto kwake ni mmoja kati ya washiriki wa Mkutano huo.(Picha na MARY GWERA, Mahakama ya Tanzania).

Wajumbe wengine walioshiriki katika paneli ya majadiliano ya mada hiyo nao pia walitoa uzoefu wao kuhusu Dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba katika nchi zao.

Mkutano huo unaoendelea hadi tarehe 03 Novemba, 2024 umebeba kauli mbiu isemayo; ‘Utu wa binadamu kama thamani ya msingi na kanuni: Chanzo cha tafsiri ya kikatiba, ulinzi wa haki za msingi za binadamu na utekelezaji.’

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news