KATAVI-Mlezi wa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt.Mohamed Said Dimwa amewasihi wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Katavi kujitokeza kwa wingi kwenda kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Ni kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuwapigia kura za ndio wagombea wote wanaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.
Rai hiyo ameitoa leo wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi wa mkoa huo wakati akifungua kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa upande wa chama hicho huko Wilaya ya Tanganyika Kata ya Ikola, Kijiji cha Mchangani,Kitongoji cha Kajinga Uwanja wa Like Tanganyika 'A'.
Katika maelezo yake, Dkt.Dimwa, amewasisitiza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuweka kando tofauti zao za makundi yaliyojitokeza katika uchaguzi wa ndani wa kura za maoni na badala yake wabaki na kundi moja la CCM linalounga mkono wagombea wateule ili upatikane ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.
Dkt.Dimwa alisema, CCM ina sababu na dhamira ya dhati ya kupata ushindi mkubwa kutokana na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 1.3 katika Mkoa wa Katavi.