ZANZIBAR-Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Joseph J. Kilangi amesema ni muhimu kuendeleza ushirikiano na Wizara ya Nishati ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania ili kuendelea kujadili mambo mbalimbali yanayohusu wizara hizo.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi kati ya Wafanyakazi wa Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar na Wizara ya Nishati ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi wa wizara hiyo Maisara.
Kilangi amesema, kuwepo kwa mashirikiano hayo itapelekea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika majukumu ya kazi za kila siku.
Aidha,amesema kufanyika kwa kikao hicho kutasaidia kupanga mikakati mbalimbali kwakuangalia maeneo yanayoweza kuzalisha nishati ya umeme ili kuwa na umeme wa uhakika nchini.
Akizungumzia kuhusu nishati safi ya kupikia amesema, kadri vikao hivyo vitakapoendelea, watendaji watajadili jinsi ya upatikaji na usambazaji wa nishati hiyo ili iweze kukubalika kwa wananchi na kuwafikia kwa haraka watumiaji vijijini Unguja na Pemba.
Hata hivyo, amefafanua kuwa kikao hicho kitawawezesha watendaji kupanga mpango mkakati wa mwaka mzima wa utekelezaji ikiwemo kufanya tafiti za mawimbi ya bahari ya kuzalisha umeme pamoja na kusambaza mtambo wa gesi kutoka bara.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhandisi Felchesmi Mramba amesema jinsi ya kuendeleza mashirikiano kati ya wizara hizo ni kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi hizo kwa wananchi.
Hata hivyo, ameeleza katika kikao hicho kutasaidia utekelezaji wa miradi ambayo inahusiana na taasisi hizo hasa kwenye takwimu za upepo wa umeme wa gesi kwa upande moja na kwa upande wa mafuta na gesi ili kuweza kuziratibu na kuzifanyia kazi.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamesema, wataendeleza mashirikiano hayo kunufaika na vitu mbali mbali ikiwemo kubadilishana uzowefu wa kazi na kujua jinsi ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika kazi zao sambamba na kutambua mifumo mbali mbali ya nishati pamoja na gesi.
Kikao hicho cha siku mbili ambacho kimewashirikisha wakurugenzi, watumishi maafisa mipango na wafanyakazi mbalimbali waliomo ndani ya taasisi katika wizara hizo.