ARUSHA-Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umepitisha Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo ikiwa ni miongoni mwa lugha tatu rasmi zitakazotumika katika shughuli za Jumuiya ya EAC ambazo ni Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili.
Akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto amesema kuwa, Kiswahili kama lugha inayowaunganisha waafrika inaelezea utamaduni wa pamoja kama wana Afrika Mashariki na kinategemewa sana kutokana na wananchi wengi katika jumuiya kuelewa lugha ya Kiswahili ukilinganisha na lugha nyingine.
Amesema kwamba, kupitishwa kwake kama lugha rasmi kutawawezesha wananchi kufuatilia vikao rasmi ambavyo vitaendeshwa kwa lugha wanayoielewa, kutarahisha ufanyaji biashara na masuala mengine ya Mtangamano.
Ameongeza kusema, uamuzi huo pia utaimarisha utambulisho wa wana Afrika Mashariki katika kutangaza kikamilifu dira ya Jumuiya pamoja na kuimarisha uwezo wa wananchi katika kushirikiana ndani ya nchi zao, kikanda na duniani kwa ujumla.
Lugha ya Kiswahili na Kifaransa zitaanza kutumika kufuatia kufanyika kwa marekebisho ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya Kifungu Namba 137, ambao awali ulitambua lugha ya Kiingereza pekee. Lugha hizi sasa zitatumika kwenye vikao vyote vya Jumuiya hiyo na taasisi zake.
Kutambuliwa kwa Lugha ya Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni hatua muhimu ya kujivunia kwa Tanzania ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Kiswahili kinakua na kutambulika kikamilifu katika medani za kikanda na kimataifa.
Itakumbukwa pia kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2022 lilitangaza tarehe 7 ya mwezi Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.
Aidha, mwaka 2022 Umoja wa Afrika (AU) ulipitisha lugha ya Kiswahili, kuwa lugha rasmi ya kazi ndani ya Umoja huo, huku Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019 ikiridhia Kiswahili kama Lugha ya kazi katika Mikutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi ambao umefanyika tarehe 30 Novemba 2024, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyeji wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni,
Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Mayardit Kiir, Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia, Mhe. Hassan Sheikh Mohamud na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza.