DODOMA- Kongamano la Tano la Kimataifa la Maendeleo ya Biashara la Chuo cha Biashara (CBE) ambalo limefanyika jijini Dodoma limetajwa kuipaisha Tanzania kimataifa.
Kangamano hilo lilifunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, tarehe 22 Novemba, 2024 na lilijadili mada mahsusi nne na mada za kitafiti kuhusu biashara na uchumi 170.
Mhe. Majaliwa alimpongeza Mkuu wa Chuo hicho pamoja na wasaidizi wake kwa ubunifu mkubwa wa kuandaa kongamano hilo.
Kongamano hilo la Tano la Kimataifa la Maendeleo ya Biashara na Uchumi, liliandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) lilifanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma tarehe 22 hadi 23 Novemba,2024.
Aidha,kauli mbiu ya kongamano hilo ilikuwa, "Mazingira ya Biashara na Uwezeshaji kwa Maendeleo Jumuishi".
Bw. Derek Murusuri ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi na mwandishi wa vitabu na CEO wa Royal Publishers, akiwasilisha Mada Mahsusi ya Mchango wa 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilivyoboresha mazingira ya biashara nchini Tanzania, katika Kongamano la Kimataifa la Maendeleo ya Biashara na Uchumi.
Mojawapo ya mada mahsusi zilizowasilishwa ni pamoja na Mchango wa 4R za Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jinsi zilivyosaidia kubadilisha mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania, iliyowasilishwa na mwakilishi wa zamani wa Association of Business Executives (ABE), Bw. Derek Murusuri.
Wengine waliowasilisha mada Mahsusi ni Col. (Mstaafu), Joseph Simbakalia-Mwenyekiti wa Bodi ya TENDO, Bw. Oscar Kisanga-Mtendaji Mkuu wa TCCIA na Bw. Safari Fungo - Mtaalam wa biashara ya kimataifa.
Mwingine ni Prof. Vasileios Paliktzoglou - Mwanazuoni na Prof. Li Deng wa Sichuan Vocational College of Finance & Economics ya China.