DAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu ameibuka na kile ambacho ni kiashiria cha anguko la chama hicho.
Lissu ambaye siku za karibuni amekuwa akiibua mambo mazito ndani ya CHADEMA ikiwemo tuhuma za rushwa kwa sasa inaonekana amekata tamaa na mwelekeo wa chama hicho kwa sasa. Huu ni ujumbe wake katika kundi sogozi la WhatsApp CHADEMA Kaskazini.
"Hii hoja haina mashiko yoyote kwenye logic na kiuhalisia. Vyama vya siasa hushiriki uchaguzi kwa kutegemea mazingira ya kisiasa ya nchi husika na malengo ya chama chenyewe.
"Chama cha siasa chenye malengo ya kushika dola ili kufanya mabadiliko ya msingi katika siasa, uchumi na jamii lazima kipiganie kwanza mabadiliko ya msingi ya mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
"Kisipofanya hivyo, badala yake kikaamua kushiriki kila aina ya uchaguzi, basi hakitakuwa na future yoyote. Kitakufa a natural death. Mifano ni mingi katika Afrika hii na katika Tanzania hii.
"ANC ya Afrika Kusini haikushiriki uchaguzi wowote kuanzia ilipoanzishwa mwaka 1912 hadi mwaka 1996 ilipopatikana Katiba Mpya ya kidemokrasia ya nchi hiyo. Je, hakikuwa chama cha siasa???.
"Hata ZANU-PF ya Robert Mugabe na ZAPU ya Joshua Nkomo wa Zimbabwe, navyo havikushiriki uchaguzi wowote kuanzia vilipoanzishwa miaka ya mwanzo ya '60 mpaka ilipopatikana Katiba Mpya ya Uhuru ya '79/'80. Hivi navyo havikuwa vyama vya siasa???.
"Kwa upande mwingine, ZANU-Ndonga ya Padre Ndabaningi Sithole na UANC ya Askofu Abel Muzorewa vilishiriki kila uchaguzi ulioitishwa na serikali ya Ian Smith. Vyote viliishia kwenye jaa la taka la historia.
"Funzo la historia ni kwamba ukiweka msimamo kwamba chama chako kitashiriki uchaguzi wowote ule 'no matter what', basi ujue umewapa leseni maCCM kutokukubali mabadiliko yoyote ya kikatiba, kiutendaji na kisheria kuhusu mfumo wa uchaguzi.
"Aidha, unakuwa umekubali na kuhalalisha kila aina ya uchafu utakaofanyiwa kwenye uchaguzi huo. Na utafanyiwa uchafu kweli kweli.
"Matokeo yake ni kwamba wananchi watakata tamaa, chama kitapoteza support ya wanachama na wananchi na kitasinyaa na kufa kama vilivyokufa vyama vingine vyote mnavyovifahamu ambavyo vimekubali kucheza ngoma ya uchaguzi ya maCCM.
"Once upon a time, UDP ya John Cheyo na CUF ya Prof. Ibrahim Lipumba vilikuwa na wabunge wengi zaidi ya CHADEMA.
"Leo, baada ya kukubali kushiriki na kuhalalisha kila uchaguzi wa nchi hii, vyama hivyo vimebaki makasha na majina tu.
"Huko ndiko mnakotaka na sisi tuishie???.Mimi binafsi sikubaliani na msimamo wa aina hii. Kama tulihitaji kuona ili tuamini, kama Tomaso wa kibiblia, basi chaguzi za '19, '20 na sasa '24 zimetuonyesha wazi aina ya challenge tuliyonayo.
"Sasa tuna uamuzi wa kufanya: tuwe kama UDP ya John Cheyo na CUF ya Prof. Lipumba, au tuwe CHADEMA ya People's Power ya kweli badala ya maneno na geresha tu.
"Mimi nachagua kuwa CHADEMA ya People's Power ya kweli. Ni mapambano mbele kwa mbele mpaka kieleweke!!!.
"Unataka Katiba ya kupewa kaka Baraka??? Kama ya kupewa ni hii tuliyo nayo sasa. Katiba ya kidemokrasia ya wananchi itapiganiwa. Haitatolewa kwenye beseni!!!,"amesisitiza kwa kina Tundu Lissu.
Haya yanajiri ikiwa ndani ya chama hicho kuna fukuto kubwa,kwani licha ya viongozi mbalimbali mikoani kuhama kimya kimya, pia zimekuwa zikipigwa ngumi za wazi wazi ili watu waweze kutetea maslahi yao.
Miongoni mwa matukio ambayo yaliwashangaza wengi siku za karibuni ni pamoja na vurugu zilizotokea katika uchaguzi wa viongozi wa chama Mkoa wa Arusha hivi karibuni ambapo wanachama walichapana kisawasawa.
Tags
Habari