Maamuzi yenu katika sanduku la kura kesho yataheshimiwa-Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema kila kura ambayo itapigwa kesho kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji ina maana kubwa kwa jamii na Taifa.
Mhesimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Novemba 26,2024 wakati akihutubia Taifa lkutokea Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kesho Novemba 27,2024 huku akisisitiza maamuzi yao yataheshimiwa.

Kutokana na umuhimu wa uchaguzi huo kwa taifa, tayari Rais Dkt.Samia alishatoa tamko rasmi kuwa kesho itakuwa siku ya mapumziko nchini ili kila aliyetimiza vigezo akashiriki uchaguzi huo kikamilifu.

“Ndugu wananchi kesho Jumatano Novemba 27,2024 ni siku ambayo tutaendeleza utamaduni wetu wa kupata viongozi wetu kwa njia ya uchaguzi.

"Tutawachagua viongozi wetu wa mitaa,vijiji na vitongoji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hii ni fursa muhimu kwa kila Mtanzania mwenye fursa ya kupiga kura kuchangia maendeleo ya nchi kwa njia ya kidemokrasia, kwa kuchagua kiongozi mwenye sifa.

"Ndugu wananchi kila kura itakayopigwa ina maana na itasaidia kufanikisha azma yetu ya kujenga jamii yenye haki, usawa na maendeleo kwa wote.

"Uchaguzi ni haki yetu na ni jukumu letu kuhakikisha tunatumia haki hiyo kwa amani na utulivu, hivyo niwasihi wananchi tujiepushe na vitendo vya uchochezi, vurugu au uvunjifu wa sheria."

Amesema Rais Dkt.Samia huku akisisitiza kuwa,amani ni urithi wetu wa thamani na ni wajibu wetu kuilinda kwa gharama yoyote ile.

"Aidha ni muhimu kuheshimu maamuzi ya wapiga kura, kwani demokrasia yenye nguvu hujengwa kwa misingi ya heshima na mshikamano.

"Niwakumbushe wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura kuhakikisha wanajitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba.

"Niwasihi chagueni viongozi waadilifu, wabunifu na wenye maono ya kuendeleza jamii zetu, kumbukeni kila kura ina umuhimu mkubwa katika kuamua mustakabali na maendeleo yetu na Taifa kiujumla."

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa na wagombea.

“Kwa viongozi wa vyama vya siasa,wagombea na wasimamizi wa uchaguzi niwakumbushe kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi, na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau.

"Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi zilizopo, nitoe rai kwa kila ndau wa uchaguzi huu kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma ya kuwa na uchaguzi wa amani unaoakisi heshima yetu kama Taifa lenye mshikamano na demokrasia imara."

Rais Dkt.Samia amesema,vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 2 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni nchini kote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news