Maandalizi ya ziara ya Rais Dkt.Samia nchini Cuba yapamba moto

HAVANA-Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo wameongoza kikao cha Ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliowasili Havana nchini Kuba kwa ajili ya maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba, 2024.
Kikao cha maandalizi kilichofanyika tarehe 2 Novemba, 2024 jijini Havana ambacho muendelezo wa maandalizi ya ziara hiyo yaliyoanza na ukaguzi wa maeneo yatakayohusika wakati wa ziara ikiwemo: Maandalizi ya ukumbi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili na Bustani ya Mashujaa (Heroes Park).Ziara hiyo pamoja na masuala mengine, itaangazia zaidi ushirikiano wa uwili na changamoto za ulimwengu zinazohitaji suluhisho la pamoja kwa maslahi ya pande zote. Pia, inalenga kuziwezesha Tanzania na Kuba kuendelea kukuza uhusiano wake wa kihistoria na kidiplomasia kuwa wa kimkakati kwa kufungua maeneo mapya ya ushirikiano yenye maslahi kiuchumi na kijamii.

Kwa muktadha huo, Tanzania imejipambanua kukuza ushirikiano wake na Kuba mathalani katika maeneo ya afya, elimu, sanaa, michezo, utalii, lugha ya Kiswahili na kuvutia uwekezaji hususan katika eneo la uchumi wa buluu.
Akiwa nchini humo, Mhe. Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Miguel Díaz-Canel Bermudez, Rais wa Jamhuri ya Kuba tarehe 7 Novemba, 2024.

Vilevile, atapata wasaa wa kuweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu la José Martí Memorial ikiwa ni ishara ya kumuenzi shujaa huyo wa taifa la Kuba na kuzindua sanamu la Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika eneo maalum la Mashujaa wa Afrika na Waasisi wa Mataifa lililopo jijini Havana.
Aidha, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na Mheshimiwa Rais Dkt. Bermúdez watashuhudia utiaji saini wa kumbukumbu za pamoja za ziara, Hati ya makubaliano baina ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Kikomunisti cha Cuba (CDC).

Tarehe 8 Novemba, 2024 Rais Samia atakuwa mgeni rasmi na kufungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili na baadae viongozi hao watafanya ufunguzi rasmi wa Kamusi ya Kispanyola na Kiswahili na kitabu cha maneno na misemo ya kila siku ya Kispanyola na Kiswahili kilichoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Havana ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa kati ya taasisi hizo mwezi Septemba, 2023.
Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba katika kutangaza utamaduni wa Mtanzania na lugha ya Kiswahili nchini humo, Ukanda wa Caribbean na Amerika ya Kusini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news