MWANZA-Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imemwachia huru aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Simiyu, Dkt.Yahaya Ismail Nawanda baada ya kukutwa hana hatia.
Awali, Dkt.Nawanda ilidaiwa alimwingilia kinyume na maumbile mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine jiji Mwanza.
Dkt.Nawanda alikuawa akikabiliwa na kesi ya jinai namba 1883/2024 ambapo hukumu yake imesomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Erick Marley.
Ilidaiwa kuwa,mtuhumiwa alitenda kosa hilo Juni 2, 2024, majira ya saa 20:30 katika maegesho ya magari ya baa maarufu ya THE CASK iliyopo jijini Mwanza.
Dkt.Nawanda inadaiwa alimwingilia kinyume na maumbile mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye jina linahifadhiwa aliyekuwa akisoma Shahada ya Kwanza ya Ugavi na Manunuzi katika chuo hicho jijini humo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Erick Marley akisoma hukumu hiyo leo amesema, baada ya kupitia ushahidi uliyotolewa na mashahidi 11 umebaini kuwa mlalamikaji ushahidi wake umekinzana na mashahidi wa utetezi.
Aidha,kutokanana na ushahidi huo kutokidhi vigezo, mahakama hiyo imemuachia huru mtuhumiwa huyo baada ya kumkuta hana hatia ambapo upande wa mlalamikaji una haki ya kukata rufaa.