NA LUSAKO MWANG'ONDA
Mahakama Iringa
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Danstun Ndunguru ameongoza mafunzo kwa Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya za Mikoa ya Iringa na Njombe ya kushughulikia mashauri ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba, 2024.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (kulia) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kushughulikia mashauri ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yaliyotolewa jana tarehe 08 Novemba, 2024 kwa Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Iringa (hawapo katika picha). Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Richard Mkongwa.
Mafunzo hayo maalum yameratibiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa yakiwa na lengo la kuwaweka sawa Mahakimu wa Kanda hiyo kuhusu usikilizaji na uamuzi wa mashauri ya namna hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo jana tarehe 08 Septemba, 2024, Mhe. Ndunguru alisema, “tumelazimika kuitisha mafunzo haya ya siku moja ili kuwekana sawa katika kushughulikia kesi za uchaguzi. Wote tunafahamu kuwa hivi karibuni tutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo ni budi kukumbushana baadhi ya mambo katika ushughulikiaji wa kesi za namna hii ili tuwe na usawa katika uendeshaji wa kesi hizo kama zitakuwepo.”
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dustan Ndunguru (hayupo katika picha) alipokuwa akifungua mafunzo kuhusu usikilizaji wa mashauri ya uchaguzi yaliyotolewa kwa Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Iringa.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazetha Maziku akizungumza wakati akimkaribisha Jaji Mfawidhi kufungua mafunzo hayo, alisisitiza juu ya umuhimu wa mafunzo hayo kwa Mahakimu ambapo alisema kuwa, “katika uchaguzi mambo mengi hutokea, hivyo tunajiweka sawa ili kuwa na weledi sahihi katika uendeshaji wa mashauri ya kiuchaguzi kama yataletwa mahakamani.”
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo, ambapo Wawasilishaji wa mada hizo walikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Danstun Ndunguru, Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Bernazetha Maziku na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mhe. Honorious Kando.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dastun Ndunguru (aliyesimama) akiwasilisha mada kwa Mahakimu/washiriki wa mafunzo hayo.
Baada ya mafunzo hayo Mhe. Ndunguru aligawa vitabu na machapisho mbalimbali kwa washiriki wa mafunzo hayo. Nyaraka hizo ni pamoja na Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji.
Vitabu vingine vilivogawiwa kwa washiriki ni Kitabu cha Mwongozo wa Uchaguzi wa Viongozi wa Vijiji, Vitongoji utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 na Kitabu cha Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mhe. Honorious Kando akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa (kushoto) akigawa machapisho na vitabu mbalimbali kwa washiriki wa mafunzo hayo. Katika picha, Mhe. Ndunguru akimkabidhi Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Mhe. Anael Edward Uphoro (kulia).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dunstan Ndunguru (katkkati) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo kuhusu ushughulikiaji wa mashauri ya uchaguzi (waliosimama nyuma). Walioketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mhe. Honorious Kando.
Washiriki wa mafunzo hayo wameushukuru Uongozi wa Mahakama Kanda ya Iringa kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wamesema yamewasaidia kuwajengea uwezo wa uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi na hasa wa Serikali za Mitaa. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini unatarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.