Marais nane kukutana Arusha maadhimisho ya miaka 25 ya EAC

ARUSHA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye maadhimisho ya miaka 25 ambayo yatafanyika Novemba 29 hadi 30,2024.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi wanachama nane ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jamhuri ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda ayasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na viongozi wa dini mkoani Arusha.

RC Makonda alisema, uwepo wa marais hao nane wa Jumuiya ya EAC ni muendelezo wa mikutano mingi ya Kimataifa na Kitaifa inayofungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani.

Rais Samia pia kando ya mkutano huo anatarajiwa kukutana na viongozi wa jamii ya Kimasai kutoka wilayani Ngorongoro mkoani hapa ili kujadiliana na kuzungumza nao katika kutafuta maridhiano.

Ni dhidi ya mgogoro uliopo baina yao kutokana na zoezi linalofanywa na Serikali la kuwaondoa ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

EAC

Kenya, Uganda na Tanzania zina historia ndefu ya ushirikiano wa kiutamaduni, kijamii na kiuchumi. 

Ingawa hapo nyuma ushirikiano huu ulianzishwa kwa faida ya utawala wa kikoloni wa Kiingereza, ushirikiano huo wa kikoloni ndio uliojenga msingi, wa ushirikiano mpya wa baadaye wa nchi huru za Afrika Mashiriki.

Aidha,kufuatia kupata uhuru kwa nchi zote tatu katika nusu ya kwanza ya miaka ya 1960 maslahi ya kiutamaduni, kijamii na kiuchumi ndiyo yalikuwa nguzo ya ushirikiano baina ya nchi hizo za Afrika Mashariki.

Taasisi ya kwanza iliyoundwa na nchi huru za Afrika Mashariki kusimamia ushirikiano baina yao ni jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilianzishwa mwaka 1967 na makao makuu ya jumuiya hiyo yalikuwa Arusha, Tanzania. 

Kwa bahati mbaya jumuiya hiyo ilivunjika mwaka 1977 ambapo kuvunjika kwa jumuiya hiyo kulitokana na sababu nyingi. 

Mojawapo ni tofauti za kisiasa, kiitikadi na mifumo ya uchumi baina ya nchi wanachama. 

Kenya iliendelea na mfumo wa uchumi huria iliourithi kutoka katika uchumi wa kikoloni,Uganda na Tanzania zilianzisha mifumo mipya ya uchumi uliomilikiwa na Serikali.

Sababu nyingine zilizochangia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashiriki ni pamoja na ukosefu wa utashi wa kisiasa baina ya viongozi, kutoshiriki kikamilifu kwa sekta binafsi na raia kwenye shughuli za ushirikiano, na kutokuwapo kwa usawa katika kugawana matunda ya jumuiya baina ya nchi wanachama. 

Hali hii ilisababishwa na tofauti ya viwango vya maendeleo baina ya nchi wanachama. Wakati Kenya iliendelea kiviwanda, Uganda na Tanzania zilikuwa ni soko kwa bidhaa zilizokuwa zikizalishwa Kenya. 

Kutokuwapo na sera maalum za kurekebisha tofauti hizi kulichangia, kwa kiasi kikubwa, kuvunjika kwa jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki.

Kufuatia kuvunjika kwa jumuiya mwaka 1977, nchi wanachama ziliajiri mpatanishi ambaye alihusika katika kugawa mali na madeni ya jumuiya baina ya nchi wanachama. 

Kazi hii ilifanyika katika kipindi cha miaka saba, yaani toka 1978 mpaka 1984, wakati nchi wanachama walipoweka saini Makubaliano ya Upatanishi.

Makubaliano ya Upatanishi yalisainiwa Arusha, Tanzania, Mei 24, 1984. Miongoni mwa vipengele vya Makubaliano ya Upatanishi, kimojawapo kilikuwa ni makubaliano ya kuangalia upya maeneo ambayo nchi za Afrika Mashariki zingeweza kushirikiana tena katika siku za baadaye. 

Aidha,juhudi zilianza na makubaliano ya Novemba 30, 1993 ya kuanzisha Tume ya Kudumu ya Ushirikiano ili ihusike na uratibu wa masuala ya kiuchumi, kijamii,kiutamaduni, kiusalama na kisiasa. 

Makubaliano ya uanzishaji wa Sekretariati ya Tumeya Kudumu ya Ushirikiano yalitiwa saini Navemba 26, 1994.

Baada ya kutathmini hatua zilizochukuliwa na tume katika kuendeleza ushirikiano,viongozi wa Afrika Mashariki walifikia uamuzi, huko Arusha, Tanzania, wa kuanzisha tena Jumuiya mpya ya Afrika Mashariki. 

Hivyo waliagiza Tume kushughulikia majadiliano juu ya Mkataba wa Jumuiya hiyo mpya ya Afrika Mashariki.

Matayarisho ya ufufuaji wa Jumuiya mpya yalikamilika mwaka 1999. Mkataba wa Jumuiya mpya ya Afrika Mashariki ulisainiwa na viongozi wa nchi za Afrika Mashariki Arusha, Novemba 30, 1999. Jumuiya ya Afrika Mashariki ilifufuliwa upya Julai 7, 2000.

Miongoni mwa malengo makuu ya EAC ni kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi wanachama, kuondoa vikwazo vya kibiashara, na kukuza mfumo wa biashara wa pamoja.

Pia,nchi wanachama zinashirikiana katika masuala kama vile usalama, utawala wa sheria, na kukuza demokrasia.

Vilevile, EAC inashughulikia maendeleo ya miundombinu kama vile barabara, reli, na viwanja vya ndege ili kuunganishwa kwa karibu zaidi nchi wanachama.

Aidha,lengo la muda mrefu la EAC ni kuunda umoja wa kisiasa ambao utawawezesha wananchi wa nchi wanachama kushiriki katika maamuzi ya kikanda.

Jumuaiya ya Afrika Mashariki pia, inajitahidi kukuza ushirikiano katika elimu, utamaduni, afya, na masuala mengine ya kijamii.

Katika hatua nyingine,EAC inafanya kazi ya kukuza umoja na maendeleo katika kanda hiyo, kwa matumaini ya kuleta ustawi na maendeleo kwa wananchi wanaoishi katika nchi hizo.

Licha ya mikakati thabiti,changamoto kama vile tofauti za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinakabili jumuiya hii na zinahitaji kushughulikiwa ili kufikia malengo yake kwa haraka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news