DAR-Mtumishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Eben-Ezery Mende amejitokeza kugombea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Akizungumza na DIRAMAKINI jijini Dar es Salaam, Mende alisema amewiwa kuigombea nafasi hiyo kwa kuwa uongozi ni karama aliyotunukiwa na Mungu na anaamini ataitendea haki nafasi hiyo.
"Si kila mtu ana karama ya uongozi na waliopewa karama hiyo wasipoitendea kazi watadaiwa siku ya mwisho. Mungu alienipa tunu hiyo ndiye atakaehusika ndani yangu," alisema Mende.
Uchaguzi huo utafanyika jijini Dodoma Novemba 14,mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mende, TUCTA ni taasisi kubwa inayohitaji umakini mkubwa kiuongozi na kwa namna alivyojipima amejiridhisha kwamba ataiongoza vema na kuweka historia nzuri ya kiuongozi.
Mende amewahi kuwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri (TUICO) Mkoa wa Shinyanga.