PORT LOUIS (Novemba 9,2024)-Wakati wananchi wa Mauritius wanajiandaa kupiga kura Novemba 10, 2024, kumchagua Waziri Mkuu na Kiongozi wa Serikali pamoja na Wabunge, Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SEOM), inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, imekutana na wadau mbalimbali wa siasa, ili kuhakikisha kuwa mwenendo wa uchaguzi nchini humo unafanyika kwa uwazi na amani.
Miongoni mwa wadau muhimu waliokutana na Misheni ya SEOM ni Misheni za Uangalizi wa Uchaguzi za Kimataifa za Umoja wa Afrika, Umoja wa Nchi Zinazozungumza Kifaransa pamoja na Jukwaa la Uangalizi wa Uchaguzi wa Kusini mwa Afrika; ambao wote wamewasili nchini humo kufuatilia kwa karibu uchaguzi mkuu utakaochagua Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye ndiye kiongozi wa Serikali pamoja na Wabunge.
Akizungumza katika mkutano na wadau hao muhimu Mhe. Othman alisisitiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kama Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama; ya kusimamia mchakato wa chaguzi zinazoendelea kwenye nchi wanachama wa SADC, na kuzishukuru mamlaka za Mauritius pamoja na Misheni za Uangalizi wa Uchaguzi za Kimataifa wanaoshiriki katika zoezi hili la kidemokrasia kwa ajili ya maendeleo ya nchi za bara la Afrika.
Mara baada ya kuwasili nchini Mauritius, Mheshimiwa Chande, ambaye pia ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na wanachama wengine wa SADC-TROIKA kutoka Malawi na Zambia na kwa msaada wa Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC (SEAC) lililowakilishwa na Tanzania na DRCongo, kiongozi huyo amekutana na wadau mbalimbali, kwa lengo la kukusanya maoni yatakayosaidia kwenye tathmini na mapendekezo ya SEOM kuhusu uchaguzi huo.
Baadhi ya Wadau hao ni Wizara, Idara, Taasisi na Wakala wa Serikali ya Mauritius, Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Vyuo Vikuu, na Jumuiya ya Wanadiplomasia.
Wizara, Idara, Taasisi na Wakala wa Serikali
Misheni ya Mhe. Chande na ujumbe mzima wa SEOM, SEAC na SADC TROIKA ilikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Maneesh Gobin, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda, na Biashara ya Kimataifa ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Mauritius.
Timu hiyo pia ilikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Anil Kumar Dip, Kamishna wa Jeshi la Polisi la Mauritius, ambapo misheni ilipata fursa ya kujadili hatua za usalama zilizowekwa katika kipindi cha uchaguzi, siku ya kupiga kura na siku ya kuhesabu kura, utaratibu ambao umewekwa kikatiba nchini humo.
Ujumbe wa SADC pia ulipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Tume ya Uchaguzi, ambapo walipokea taarifa za kina juu ya maandalizi ya uchaguzi na mfumo wa vifaa vilivyowekwa kuhakikisha mchakato wa kupiga kura unafanyika kwa uwazi.
Taasisi nyingine za Serikali zilizokutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa SADC chini ya Mhe. Chande ni Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Utangazaji la Mauritius (MBC) na Kitengo cha Habari cha Serikali.
Mazungumzo ya Misheni na wawakilishi wa taasisi hizo yalilenga kujua mwenendo mzima wa utoaji Habari kwa umma na usambazaji wa taarifa za uchaguzi kwa umma kupitia chombo cha Habari cha Taifa.
Ujumbe wa SADC pia ulipata fursa ya kuzungumza na vyama vya siasa nchini Mauritius ambapo viongozi wa kisiasa kutoka Linion Reform (Chama cha Mageuzi), wakifuatiwa na Chama cha Alliance du Changement (Muungano wa Mabadiliko), na Chama cha Alliance Lepep (Muungano wa Watu) walishiriki.
Katika mikutano hii, wawakilishi wa kisiasa walitoa maoni yao juu ya mazingira ya uchaguzi na matarajio yao kuwa na uchaguzi wa amani na wenye matokeo yanayoakisi uhuru na haki.
Viongozi wa Dini, Vyuo Vikuu, na Kundi la Kidiplomasia
Misheni ya SADC chini ya uongozi wa Mhe. Chande pia ilikutana na viongozi wa Baraza la Dini la Mauritius, ambapo wawakilishi walieleza jukumu la jumuiya za kidini katika kukuza amani na kuhimiza ushiriki wa raia kwenye zoezi la kura.
Mkutano mwingine ulifanyika baina ya Misheni ya SEOM na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Mauritius na ambapo walitoa mitazamo yao ya kitaaluma na kitafiti kuhusu mchakato wa uchaguzi nchini humo.
Katika hatua nyingine muhimu ya kushirikisha wadau, Misheni pia ilikuatana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Wanadiplomasia iliyojumuisha wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa na Wawakilishi kutoka nchi wanachama wa SADC wanaoishi Mauritius. Mazungumzo yao yalijikita kwenye ushirikiano wa kimataifa uliopo miongoni mwao katika kusaidia dhamira ya Serikali ya Mauritius ya kufanikisha uchaguzi wa amani na ulio huru.
Misheni za Uangalizi wa Uchaguzi za Kimataifa
Katika kikao chake na Misheni za Uangalizi wa Uchaguzi za Kimataifa, ambacho kilihitimisha mikutano ya wadau, Mhe. Chande alieleza matumaini yake kwamba Mauritius itadumisha sifa yake ya kufanya uchaguzi wa amani na ulio huru kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Uchaguzi wa kesho utakuwa muhimu kwa watu wa Mauritius, na SEOM iko hapa kushuhudia, kuripoti, na kuunga mkono matarajio ya kidemokrasia ya taifa hili. Tuna imani kwamba wadau wote wataendelea kukuza mazingira yanayoheshimu matakwa ya wananchi,” alisema.
Mhe. Chande ataongoza ujumbe wa SEOM kutembelea maeneo mbalimbali nchini siku ya uchaguzi ili kufuatilia kwa karibu zoezi la upigaji kura.
Taarifa ya awali ya SEOM kuhusu mwenendo wa uchaguzi itatolewa tarehe 13 Novemba 2024, katika Kituo cha Sanaa cha Caudan mjini Port Louis, ambapo wawakilishi wa kidiplomasia na vyombo vya habari wamealikwa kuhudhuria.
Ushiriki wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SEOM) nchini Mauritius unathibitisha kuwepo na dhamira ya dhati ya kudumisha misingi ya kidemokrasia na mabadiliko ya uongozi kwa amani ndani ya Jumuiya ya SADC.
Aidha uongozi mahirii wa Mhe. Chande na msimamo wa SEOM usioegemea upande wowote unaonyesha dhamira ya SADC katika kudumisha uadilifu wa kidemokrasia ndani ya kanda na kupigiwa mfano ndani ya Afrika na duniani.
Wakati Mauritius ikielekea kwenye uchaguzi, uwepo wa SEOM unaashiria mshikamano baina ya nchi wanachama na wananchi wa Mauritius katika safari ya kidemokrasia.