ARUSHA-Marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameshiki Mjadala wa Wakuu wa Nchi katika maadhimisho ya miaka 25 ya jumuiya hiyo.
Mjadala huo umefanyika leo Novemba 29,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametaja mabadiliko ya tabianchi kama changamoto kubwa ya kimataifa.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, kwa sasa mabadiliko ya tabianchi ni wimbo ambao kila nchi inauimba huku akibainisha kuwa rasilimali zilizopo hazitoshi kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema, zinapaswa kuchukuliwa hatua za dharura ikiwemo upandaji miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yameendelea kuleta matokeo hasi kwa jamii, kitaifa na Kimataifa.
Pia, Rais Dkt.Samia ameeleza umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo yote yatawezekana ushirikiano wa sekta zote.
Vilevile Rais Dkt.Samia ameweka wazi dhamira yake ya kuboresha maisha ya wanawake kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi za kupikia kwa kulinda mazingira na afya za wananchi.
Naye Rais wa Jamhuri ya Uganda,Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni amezungumzia suala la biashara ya mchele huku akibainisha kuwa,alikataa shinikizo la kuweka zuio la mchele wa Tanzania kuingia nchini Uganda, akisema kuwa hatua hiyo haikuwa sahihi.
Amesema kuwa,alikataa kwa sababu hatua hiyo ilikuwa inalazimisha Waganda kununua mchele ghali zaidi, jambo ambalo lingewaumiza kiuchumi.
Pia,Rais Museveni amesisitiza kuwa, zuio hilo lingeharibu juhudi za wakulima wa Tanzania ambao hutegemea soko la kikanda kuuza mazao yao.
Kiongozi huyo ameonesha msimamo wake wa kuunga mkono soko huria, akisema wakulima wanapaswa kushindana badala ya kulindwa na vizuizi vya kibiashara, kwani ushindani huchochea wakulima kuboresha ufanisi na ubora wa bidhaa zao.
Katika hatua nyingine, Rais Museveni ameonesha kusikitishwa na namna Waafrika wanaendelea kubaki nyuma huku wenzao wa Magharibi na Asia wakiendelea kupenya hadi mwezini.
“Wamarekani wanaenda kwenye mwezi, sisi tupo tu. China, wanaenda kwenye mwezi, Urusi wanaenda kwenye mwezi na hivi karibuni India wanaenda kwenye mwezi."
Rais Museveni ameonesha umuhimu wa Waafrika kuongeza bidii katika ubunifu na teknolojia ili nao wasiachwe nyuma katika maendeleo ya Sayansi na Teknolojia duniani.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt.William Ruto ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ambayo imepiga hususani upande wa biashara.
"Kenya ilikuwa ikiongoza kwa biashara, lakini sasa Tanzania imechukua nafasi hiyo. Niwapongezeni sana Watanzania kwa hatua hiyo."