ZANZIBAR-Ili Zanzibar iendelee kubaki katika orodha ya miji ya urithi wa Dunia, elimu inapaswa kufikishwa kwa wanajamii watambue wajibu walionao katika kutunza maeneo ya hifadhi ukiwemo Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Hivyo, vyombo vya habari vina jukumu la kuhakikisha vinaandaa vipindi na makala mbalimbali zinazoelimisha umma juu ya uhifadhi huo kwa manufaa ya sasa na baadae.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uhifadhi Mji Mkongwe (JUHIMKO),Dkt. Maryam Jaffar Ismail, katika semina ya siku moja kwa waandishi wa habari iliyofanyika Forodhani kuwataka watumie nafasi yao kufikisha elimu kwa jamii.
Dkt.Mariam alisema, bila mchango wa waandishi wa habari, juhudi za kuepusha Mji Mkongwe na hatari ya kutolewa katika orodha ya miji ya urithi wa Dunia inayosimamiwa na UNESCO zinaweza kushindwa.
Alieleza kuwa, majengo ya mji huo yanakabiliwa na uchakavu mkubwa unaohitaji kumshirikisha kila mtu, taasisi za Serikali na kiraia, kusaidia kuubakisha katika uasili na mvuto wake.
Alisema, JUHIMKO ambayo ni taasisi binafsi, inaendesha mradi wa kuhifadhi Mji Mkongwe kutokana na ufadhili kutoka Uingereza, na imeweza kulifanyia matengenezo makubwa jengo lililokuwa ofisi ya ushuru zamani, Old Custom ambalo inalitumia kiofisi, na inaendelea na mradi wa kuyakarabati majengo mengine ya mji huo, kwa kutumia mafundi vijana wa kike na kiume waliowapatia mafunzo maalum.
Hata hivyo, alisema wanavitegemea sana vyombo vya habari kusaidia harakati za kutoa elimu kwa wananchi wakitambua vina nguvu kubwa na vinaweza kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.
“Mji Mkongwe ni wetu, kila mtu ashiriki kuuhifadhi tusiiachie serikali au JUHIMKO peke yao. Tushirikiane katika hili,”alisisitiza.
Aliwashauri wanahabari na wadau wengine wa Mji Mkongwe kuunda umoja utakaosaidia kuhamasisha jamii juu ya utunzaji mazingira na uhifadhi ili kuisaidia serikali katika kukabiliana na hali hiyo inayosababishwa na ongezeko kubwa la joto linalochangia kuzalisha unyevunyevu ambao ni adui mkubwa wa majengo hayo ya kale.
Makame Juma Mtwana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa JUHIMKO, alieleza kuwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri majengo, taasisi hiyo imemudu kuwahamasisha wanafunzi wa skuli zilizoko Mji Mkongwe kuunda klabu za mazingira na utunzaji urithi, ikianzia na skuli za Memon Academny, Forodhani na Mluka bint Alawi, ili kuwapa mwamko na kuleta mabadiliko chanya katika kulinda majengo ya urithi Zanzibar.
“Kama sisi tumerithi maeneo haya yakiwa na hali nzuri, ni wajibu wetu pia kuwarithisha watoto na wajukuu zetu lakini ni lazima tujue namna bora ya kuyatunza majengo yetu na kwa kutumia vifaa vya asili katika matengenezo kama vile chokaa, mawe, udongo na mbao maalum,” alisema.
Ofisa huyo pia aliisisitiza jamii ijenge utamaduni wa kupanda miti kwa ajili ya kupoza joto, pamoja na kupunguza kupitisha vyombo vya moto vyenye uzito mkubwa katika mji Mkongwe ambavyo mitetemo yake huchangia kutia ubovu majengo hayo.
Ofisa kutoka Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza waa Rais Dk. Salim Hamad Bakar, akitoa mada kuhusu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, utamaduni na urithi, alisema kubadilika kwa miongo ya mvua, hali ya hewa na masuala ya kibayolojia, kunaleta athari zisizotarajiwa na kuharibu urithi wa asili.
Alisema, utashi wa binadamu unachangia sana uharibifu kwa kupuuza maelekezo ya wataalamu kwa kisingizio cha mahitaji ya kimaisha, ndio wanapokata miti na kutupa taka ovyo katika mitaro ya kupitishia maji ya mvua.
“Tuache kuharibu mazingira yetu kwani kufanya hivyo ni kujidhuru wenyewe kisha tunasema ni tabianchi lakini tunasahau tabiawatu na kujiletea majanga ikiwemo maji ya bahari kupanda kwenye makaazi ya watu,” alisema.
Waandishi walioshiriki mafunzo hayo walishauri mamlaka zijiangalie vyema kwani licha ya kutunga sheria sera na kanuni za mazingira, baadhi ya watendaji wanatawaliwa na muhali pale wanapokamata waharibifu, jambo linalotia shaka ya kuwepo mchezo mchafu unaorudisha nyuma jitihada za kuihami nchi na maafa.