Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika wahitimishwa Zimbabwe

NA MARY GWERA 
Mahakama Zimbabwe

JAJI Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba amefunga Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) na kukiri kuwa, mkutano huo umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na mahudhurio na michango mizuri iliyotolewa na Washiriki.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akisikiliza hotuba ya kufunga Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba (hayupo katika picha).

Akifunga mkutano huo, uliofanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2024 hadi tarehe 03 Novemba mwaka huu, katika mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe, Mhe. Malaba alisema kuwa, wao kama wenyeji wamefurahishwa na mkutano huo.

“Ushiriki wa mamlaka kutoka mamlaka tofauti katika shughuli za mkutano huu ulikuwa wa kufurahisha. Tuliweza kuvunja vizuizi vya lugha na uzoefu wetu kwa heshima na majukumu yetu ya pamoja ya kutoa haki ya kikatiba kwa watu wetu,” alisema Jaji Mkuu huyo.

Alisema, mada zilizowasilishwa na wasemaji zilikuwa na utofauti na zilionesha mawazo na namna nchi mbalimbali zinavyotekeleza na kusimamia utu na haki za binadamu.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba akifunga Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) ulioanza kufanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2024 hadi tarehe 03 Novemba mwaka katika Hoteli ya Elephant mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Aidha, Jaji Mkuu huyo amesema kwamba, Mkataba wa Kongamano la Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika unathibitisha dhamira katika kukuza haki ya kikatiba barani Afrika.

“Katika suala hili, Mahakama ya Zimbabwe inajitolea kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya CJCA kama Marais wengine waliopita wamefanya na wanaendelea kufanya. Kujikita kwa utii wa katiba ni mchakato unaosimikwa katika juhudi za kuendelea kufuata kanuni zinazosisitiza,”alisema Jaji Malaba.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba (hayupo katika picha) alipokuwa akifunga Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) uliofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Wakati wa Mkutano huo, Mahakama ya Zimbabwe ilikabidhiwa Uenyekiti wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika, ambapo Jaji Mkuu huyo alitoa shukrani kwa wanachama wa CJCA kwa kuikabidhi Zimbabwe jukumu hilo muhimu.

“Nina furaha kueleza dhamira yangu binafsi na ya Zimbabwe katika kuimarisha na kuendeleza malengo ya CJCA wakati wa uenyekiti wa Kongamano hilo. Kwa Zimbabwe, kutimiza mfumo wa kikatiba ambao CJCA imeanzishwa ni ahadi ya kudumu,” alisisitiza Mhe. Malaba.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba wakati wa hafla ya kufunga Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) uliofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa pamoja na Jaji Mkuu wa Malawi, Mhe. Rizine Mzikamanda wakati wao pamoja na washiriki wengine (hawapo katika picha) wa Mkutano wa Saba wa CJCA walipotembelea maporomoko ya maji ya Victoria (Victoria Falls) yaliyopo nchini Zimbabwe.

Mada mbalimbali zilizotolewa zililenga kusimamia utekelezaji wa haki za binadamu sambamba na kuhifadhi na kuthamini utu wa binadamu. Moja ya maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ni kila Mahakama ya Kikatiba Afrika kuendelea kutoa haki kwa kuzingatia utu wa binadamu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alikuwa miongoni mwa washiriki waliohudhuria kikamilifu mkutano huo muhimu uliobeba Kaulimbiu isemayo; Utu wa binadamu kama thamani ya msingi na kanuni: ‘Chanzo cha tafsiri ya kikatiba, ulinzi wa haki za msingi za binadamu na utekelezaji.’
Katika picha ni sehemu ya maporomoko ya maji ya Victoria (Victoria Falls) walipotembelea washiriki wa Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA).
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) walipotembelea katika eneo la maporomoko ya maji ya Victoria (Victoria Falls) nchini Zimbabwe.

Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Tanzania alipata fursa ya kuwasilisha mada kuhusu ‘dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba’ ambapo alitoa rai kwa Majaji wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) kutafakari kama uamuzi wanaotoa unazingatia haki na utu wa binadamu kama inavyoeleza kaulimbiu ya mkutano wa saba wa Mahakama hizo.

Baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano huo, washiriki walipata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo mjini Victoria Falls nchini humo ambavyo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Chamabondo, Maporomoko ya maji ya Victoria (Victoria Falls) na Mto Zambezi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news