NEW YORK-Tanzania imetangazwa kuwa nchi yenye daraja la juu zaidi katika hali ya uchumi wake kupitia ithibati zinazofanywa na taasisi ya kimataifa ya Moody's.
Katika raundi ya karibuni, Tanzania imepewa daraja B1 wakati jirani zake Kenya wakipewa alama B3 huku Uganda na Rwanda wakipewa alama B2.
Vigezo hivi vya Moody ndivyo huamua uwezo wa nchi kukopeshwa na nchi au taasisi za kimataifa.
Moody's ambayo ina makao makuu jijini New York nchini Marekani ni kampuni maarufu inayotoa madaraja ya mikopo kwa serikali, makampuni, na vyombo vingine vya kifedha.
Aidha, hatua hiyo huwa inasaidia wawekezaji kujua hatari ya kukopa au kuwekeza katika taasisi fulani au nchi.
Madaraja ya Moody's yanaashiria kiwango cha uwezo wa taasisi kutimiza majukumu yake ya kifedha kama vile kulipa madeni.
Vilevile, madaraja ya Moody's hutolewa kwa alama kama Aaa, Aa, A, Baa, na kadhalika, ambapo Aaa ni kiwango cha juu cha usalama na C au D kinawakilisha hatari kubwa ya kutolipa madeni.
Kampuni hiyo hutumia mifumo maalumu ya kutathmini hatari ya kifedha, na taarifa hizo hutumika na wawekezaji, benki na taasisi nyingine kufanya maamuzi ya kifedha.