Muhimbili kutoa matibabu ya macho bila malipo kwa wananchi hawa

DAR-Jumla ya wananchi 445 wamepatiwa huduma za ubingwa bobezi za uchunguzi wa macho zinazotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikishirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu ambapo kati yao 282 sawa na 63.4% wamekutwa na changamoto za uoni hafifu, mtoto wa jicho, presha ya macho, utandu kwenye macho na magonjwa mengine ya macho.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na wananchi alipotembelea Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu kujionea hali ya utoaji huduma hizo na kueleza kuwa kati 282 waliokutwa na changamoto wananchi 151 sawa na 53.6% wamekutwa na uoni hafifu unaohitaji miwani na 131 sawa na 46.4% wamepewa rufaa kupata matibabu zaidi huku kati ya waliopewa rufaa 102 sawa na 77.9% watatibiwa MNH na 29 ikiwa ni 22.1% wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke.

Aidha, katika wananchi 131 waliopata rufaa, wananchi 58 sawa na 44.3% wana changamoto ya mtoto wa jicho wote watafanyiwa upasuaji wa kibingwa MNH kupitia tundu dogo bila malipo, 27 sawa na 20.7% wana tatizo la utandu kwenye jicho usababishwao na mzio, miale ya jua na 14 sawa na 10.7% kati yao wana presha ya macho na wengine wana matatizo mengine ya macho.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dkt. Mussa Ally Makori akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, ameushukuru Uongozi wa MNH kwa kutoa huduma hizo katika hospitali hiyo na kuomba kuendelea kushirikiana nao katika kutoa huduma mbalimbali kwa wakazi wa eneo hilo ikiwemo kujenga uwezo wa watalaam wa hospitali hiyo ambapo huduma hizo zitahitimishwa leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news