DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amefanya ziara hiyo akiambatana na Wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tarehe 08 Novemba, 2024.
Akizungumzia kuhusu mradi huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa shabaha yake ni kuona ujenzi huo unakamilika kwa haraka ili Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waweze kuhamia na kutekeleza majukumu yao katika jengo hilo.
“Ni matamanio yangu kuona ujenzi huu unakamilika kwa haraka ili watumishi wetu waweze kuhamia kwenye jengo hili jipya na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi," amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake Mhandisi anayesimamia ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutoka SUMA JKT Mhandisi Evans Mwakizi, amesema kuwa hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 69, ambapo kwasasa wanaendelea na uwekaji wa vioo, kufanya “skimming” ya kuta, kuweka lift na kujenga jengo la walinzi.