NAIROBI-Mkutano Mkuu wa Sita wa Jumuiya ya Tume za Utumishi wa Umma Afrika (AAPSCOMs) uliofanyika jijini Nairobi nchini Kenya umemchagua Mhe. Jaji (Mst) Hamisa H. Kalombola ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Tanzania (PSC) kuwa Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Tume za Utumishi wa Umma Afrika (AAPSCOMs) Kanda ya Afrika Mashariki.
Ni katika kikao kilichofanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba, 2024 katika Ukumbi wa Hoteli ya Safari Park.
Mkutano huo uliandaliwa na Serikali ya Kenya kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo na Tume ya Utumishi wa Umma ya Kenya na mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi alikuwa Mhe. Justin B.N. Muturi ambaye ni Waziri wa Utumishi wa Umma na Maendeleo ya Rasilimali Watu, Kenya.
Mkutano huo uliandamana na Maadhimisho ya Miaka 16 ya Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka 2008 kama chombo cha kubadilishana uzoefu, kushirikiana, kuweka malengo ya pamoja na kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali zinazoukabili Utumishi wa Umma Afrika.
Kauli Mbiu ya Mkutano huo ilikuwa "KUCHOCHEA MABADILIKO KATIKA UTUMISHI WA UMMA KUPITIA UBUNIFU NA MAENDELEO YA TEKNOLOJIA."(Driving Public Service delivery Transformation through Innovation and Technology);