Mwinjilisti Temba apendekeza tiba kudhibiti maghorofa kuporomoka nchini

DAR-Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amelishauri Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutengeneza sheria itakayodhibiti ujenzi wa maghorofa yasiyo na viwango nchini ambayo yanaweza kuporomoka na kuleta maafa.
Temba ametoa ushauri huo Novemba 21, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Ni wakati akitoa pole na ushauri kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kufuatia vifo na majeruhi yaliyosababishwa na kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo jijini Dar es Salaam Novemba 16,mwaka huu.

Mwinjilisti Temba ambaye amewahi kuwa Mshauri wa Rais wa zamani wa Zambia, Hayati Michael Sata ameeleza kuwa, sheria hiyo itakayotengenezwa na Bunge inapaswa kubainisha kuwa endapo ghorofa litaporomoka na kusababisha maafa ardhi ya eneo hilo itapaswa kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Amesema, kama sheria hiyo ikitengenezwa itawafanya matajiri na wahandisi kuwa makini kujenga maghorofa kwa viwango vinavyotakiwa badala ya sasa ambapo wahandisi wamekuwa wakiwaachia vijana kazi ya ujenzi huku wao wakitoa tu maelekezo na wakati mwingine kuondoka kabisa eneo la ujenzi na hivyo kusababisha ujenzi kutokuwa wa viwango.

Mwinjilisti Temba ametolea mfano wa nchi inayotumia sheria hiyo kuwa ni Nigeria ambapo jengo linapoporomoka, ardhi ya eneo hilo inataifishwa na kuwa chini ya Serikali.

Amesema kuwa, ujenzi wa maghorofa Kariakoo unahitaji umakini mkubwa kwani eneo hilo lina mchanga mwingi na maji kwani ni karibu na bahari, hivyo kama ujenzi ni chini ya kiwango mchanga hauwezi kuhimili na kulishikilia jengo hilo jambo ambalo linaweza kusababisha jengo kuporomoka na kuleta madhara makubwa.

Mwinjilisti Temba ameunga mkono kauli ya Rais Dkt. Samia ya kusema kuwa,  majengo yatakayobainika kuwa mabovu baada ya wataalamu kufanya uchunguzi yabomolewe.

"Wataalam watakaopita kukagua maghorofa ya Kariakoo wachimbe kwanza ardhi na kupima udongo kuuona, pale kuna mchanga mwingi sana. 

"Ninashauri wakati wa ujenzi, ujenzi uendane na hali ya mazingira hayo. Matajiiri wakubwa wanajenga haraka haraka sana na unakuta wahandisi wanapopewa kazi, site anaachia vijana wafanye kazi, yeye anaondoka hata katika eneo hilo. 

"Hivyo kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo unaweza kuwa ulitokana na wajenzi kutofuata maelekezo kutokana na uzembe wa wahandisi,"amesema Mwinjilisti Temba.

Hata hivyo, Mwinjilisti Temba ametoa ushauri mwingine kuwa ni kuhamisha mji wa Dar es Salaam na kuanzisha Kariakoo mpya katika Shamba la Serikali NARCO lililopo Vigwaza ambapo Serikali itatakiwa kujenga soko.

Amesema,lengo ni kuepusha matajiri kuendelea kupanua maghorofa yao kwa chini (ujenzi wa underground) ambao ni ujenzi hatarishi.

Katika hatua nyingine, Mwinjlisti Temba ameiomba Serikali kutoruhusu malori kuingia mjini na badala yake yaelekee Bandari Kavu ya Kwala, kwani kuyaruhusu hususani Ubungo kunaweza kusababisha madhara makubwa kama siku moja ikitokea mlipuko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news