NAIBU KATIBU MKUU NTONDA AWASHAURI WADAU KUTUMIA FURSA YA KUTOA MAONI VYEMA

DAR-Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Methusela Ntonda awasisitiza wadau wa kazi za ubunifu zinazolindwa na Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kutumia vyema fursa ya utoaji wa maoni kwa ajili ya Kanuni zilizowasilishwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kwa kuzingatia maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa kauli hiyo Novemba 20,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao cha kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa Sanaa, Waandishi wa Vitabu, Wachapishaji wa Vitabu pamoja na bunifu mbalimbali zinazoguswa na Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
"Natambua Kanuni zinazofanyiwa marekebisho ni Kanuni ya haki ya mauzo yanayofuatia (resale right), Kanuni ya usajili wa kazi kwa hiyari na Kanuni ya watu wenye uoni hafifu hivyo basi hakikisheni mnatoa maoni yatakayowasaidia kunufaika zaidi sababu hiyo ndiyo dhamira na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan," alisema Ndg. Ntonda.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Tanzania Bi. Doreen Sinare alifafanua kuwa utekelezaji wa kuundwa kwa Kanuni hizo ni kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki yaliyofanyika mwaka 2022.

"COSOTA imepata ufadhili wa kuunda kanuni hizi kupitia Mradi wa Mpango wa kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) unaosimamiwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji," alisema Bi. Doreen.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Emmanuel Ishengoma alitoa rai kwa Wasanii kutumia fursa hiyo ya kutoa maoni vyema sababu serikali inataka kuona wananufaika zaidi na ndiyo maana imefanya marekebisho ya Sheria hiyo ya Hakimiliki.
Pamoja na hayo naye mmoja wa wadau walioshiriki kikao hicho cha kutoa maoni Bw.Mgunga Mwamnyenyelwa aliipongeza COSOTA kwa jitihada za kupambana kutengeneza miundombinu ya kisheria itakayowasaidia Wasanii na wabunifu na kuwa wasihi wadau wenzake wa sanaa kuacha kulalamika, bali waanze kuchukua hatua na kufuata maelekezo yanayotolewa na COSOTA ili waweze kunufaika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news