Naibu Waziri Sangu aridhishwa na usimamizi bora wa fedha za TASAF mkoani Rukwa

NA LUSUNGU HELELA
Rukwa

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameupongeza Mkoa wa Rukwa kwa usimamizi bora wa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini kwa kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi inayowanufaisha walengwa wa mfuko huo.
Mhe.Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela Mkoani humo ametoa pongezi hizo leo kwa nyakati tofauti wakati alipotembelea kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa na TASAF katika Wilaya Nkasi na Kalambo.

Ameitaja miradi hiyo inayotekelezwa na TASAF ikiwemo ujenzi wa kisima cha maji katika Wilaya ya Nkasi pamoja na uanzishwaji wa shamba la miti ya mbao Wilayani Kalambo.
Akizungumzia suala la ujenzi wa kisima hicho uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni tatu hadi kukamilika kwake kimekuwa msaada mkubwa kwa kuwahudumia zaidi ya kaya 200 katika Kijiji cha Kantawa.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Sangu amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi kuhakikisha anawaleta wataalamu kutoka Wakala wa Maji vjijini ( RUWASA) ili waweze kukitambua na kukiboresha zaidi kisima hicho kwani kimeonekana kutiririsha maji katika kipindi chote cha mwaka.

“Jambo kubwa lililonileta hapa ni kufuatilia utekelezaji wa fedha za Mradi wa TASAF , mfuko huu umekuwa na programu mbalimbali, zikiwemo zile zinazolenga kaya maskini ambazo hupokea fedha, pamoja na shughuli za kujitolea ikiwemo ujenzi wa hiki kisima ambapo nimefarijika mno kujionea jinsi wananchi wanavyoisaidika kupitia kisima hiki," amesisitiza Mhe. Sangu.
Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu amepongeza mradi wa upandaji miti ya mbao lenye ukubwa wa ekari mbili uliogharimu kiasi cha Sh.milioni saba hadi kukamilika kwake ambapo mbali na miti hiyo kutarajiwa kutoa mbao ila kwa sasa eneo hilo limekuwa kivutio kikubwa, achilia mbali hewa safi inayotokana na miti hiyo.

Hata hivyo licha ya kupandwa jumla ya miche 2250 katika shamba hilo, Mhe.Sangu ametoa wito kwa Mkuu wa Wilaya , Mhe.Dkt. Lazaro Komba kuwaleta wataalamu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ili waweze kubaini chanzo cha tatizo kwani baadhi ya miche imeanza kunyauka.

Awali Mbunge wa Kalambo, Mhe. Josephat Kandege amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za TASAF zinawafikia walengwa na kuboresha maisha yao.

Baadhi ya wanufaika wa TASAF wameeleza jinsi mpango huo ulivyowawezesha kuboresha maisha yao, ikiwemo kujenga nyumba, kusomesha watoto, na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Hata hivyo,Mhe.Sangu amefafanua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha mpango wa mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi vya wanufaika wa Tasaf, hatua inayolenga kuwawezesha kiuchumi zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news