RUKWA-Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma a Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Kwela, Mhe.Deus Sangu amewataka wananchi wasisahau maendeleo wanayoyaona katika Jimbo la hilo ni kutokana na jitihada za Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwenye mkutano wa Kampeni za Serikali za Mitaa uliofanyika katika Kjiji cha Ilemba, Kata ya Kalambanzite katika Jimbo la Kwela mkoani Rukwa.
Amefafanua kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan Kata ya Kalambanzite imeimarika katika sekta ya afya, elimu, barabara, maji pamoja na umeme.
Amewataka wananchi hao kujitokeza ifikapo Novemba 27 mwaka huu ili kuchagua viongozi wenye maono na mwelekeo wa kuwaunganisha kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa ambao ni Wagombea kupitia CCM.
"Chagueni viongozi ambao wana uelewa wa matatizo na kujua namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi pasipo kujali rangi, kabila au eneo,”amesema Mhe.Sangu.
Mhe.Sangu amewaeleza Wanachi wa Kata hiyo ya Kalambanzite kuwa wana kila sababu ya kuchagua Chama chenye Sera zinazotekelezeka ambacho ni Chama Cha Mapinduzi na kuachana na vyama vingine ambavyo sera zao zimelenga kuhubiri chuki na utengano.
“Nimekuja kuwaomba mtuunge mkono kwa kupiga kura na kuchukua vijiji na vitongoji vyote,” ameomba Mhe.Sangu.