DAR-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeratibu kikao kazi kati ya ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Bavaria, Ujerumani na Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo ili kuangazia namna bora za kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kwa kupitia sekta hizo mbili.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani,Mhe. Hassan Mwamweta amesema mazungumzo baina ya nchi hizo mbili yatabainisha maeneo ya kuimarisha ushirkiano na matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa, katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya maji na kilimo nchini.
Mhe. Mwamweta amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutangaza vivutio vya uwekezaji kwani juhudi hizo zimeiwezesha Tanzania kupata matokeo mazuri katika hatua zake za ukuzaji maendeleo ya kijamii, uwekezaji na kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri,
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maji wa Taifa,Wakili Haji Nandule amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani utaiwezesha Wizara kutatua changamoto zilizopo zikiwemo upotevu wa maji, uhaba wa mita za malipo kabla ya huduma (prepaid meters’) na gharama kubwa za kemikali za kusafishia maji ambazo sehemu kubwa huagizwa kutoka nje.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Mhe. Dkt. Hussein Mohamed Omar ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje, kwa kuratibu ujio wa wafanyabiashara hao, kwani kutaiwezesha Tanzania kukuza diplomasia ya uchumi, huku ikiongeza uzalishaji bidhaa za kilimo zenye viwango stahiki katika soko la kimataifa.
Mhe. Omar amesema ushirkiano baina ya pande hizo mbili utasaidia Tanzania kupata fedha za utafiti na maendeleo ya kilimo na hivyo kuweza kuzalisha mbegu bora zitakazomudu hali ya ukame na mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kutokea duniani.
Awali, Naibu Waziri wa Uchumi, Maendeleo ya Kikanda na Nishati wa Jimbo la Bavaria, Ujerumani Mhe. Tobias Gotthardt amesema Serikali ya Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania kwa kubadilishana teknolojia za kisasa na mifumo bora ya Kilimo wanayotumia wananchi wa Bavaria, itayowezesha wakulima wa Tanzania kuinua kiwango cha uzalishaji mazao yakiwemo ya biashara na chakula hivyo kuinua uwezo wa Tanzania kulisha bara la Afrika na dunia.
Ujumbe huo wa watu 35 kutoka Jimbo la Bavaria, umeshirikisha viongozi wakuu na wataalam kutoka Serikali ya Ujerumani, watoa huduma katika sekta za maji, kilimo, mazingira, wamiliki wa viwanda na makampuni, vyama vya wakulima, na wabunge wanaoiwakilisha Serikali ya Ujerumani na upinzani.