ZANZIBAR-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetunukiwa Tuzo ya Ujenzi wa nyumba bora kwa umma na taasisi ya Dunia ya masuala ya ujenzi.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Meneja wa Habari na Uhusiano wa NHC, Bw. Muungano Saguya na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Hamis Suleiman Mwalimu, aliyemuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Sharif Ali Sharif.
Hafla hiyo iliyofanyika Novemba 2,2024 katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Zanzibar Novemba ni matokeo ya kazi iliyofanywa nchini Tanzania na Kampuni ya RAFT GROUP inayojihusisha na masuala ya ukaguzi.
Kampuni ambayo kwa niaba ya Global Construction ilifanya utafiti, uchambuzi na uchaguzi wa kampuni mbalimbali nchini Tanzania zilizofanya vizuri katika sekta ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa nyumba.
Hivyo, Shirika la Nyumba la Taifa likaibuka kidedea kwa kuwa kinara wa kuwezesha ujenzi wa nyumba bora za umma nchini Tanzania na kuwa na ubunifu katika sekta ya nyumba.