DAR-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuonyesha ubora wake katika usimamizi wa fedha baada ya kutunukiwa tuzo ya mshindi wa tatu wa Uandaaji Bora wa Hesabu kwa Mashirika ya Umma kwa kufuata viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu (International Financial Reporting Standards - IFRS). Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), CPA Adolph Kasegenya na Mgeni Rasmi CPA, Benjamin Mashauri kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha katika hafla iliyofanyika leo kwenye Kituo cha Wahasibu kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Bw. Mashauri aliwapongeza Washindi wote likiwamo Shirika la Nyumba la Taifa kwa uwazi, uwajibikaji na umahiri wake katika kuandaa taarifa za kifedha zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Alibainisha kuwa, tuzo hiyo ni kielelezo cha juhudi za Shirika hilo katika kuboresha usimamizi wa fedha, uwazi wa taarifa na uwajibikaji, hatua ambazo ni muhimu kwa mashirika ya umma katika kuimarisha imani ya wadau na kuendeleza maendeleo ya kiuchumi nchini.
Shirika la Nyumba la Taifa limeendelea kuwa mfano wa kuigwa nchini Tanzania kwa kufanikisha miradi mingi ya maendeleo ya nyumba na huduma za kijamii huku likizingatia uwajibikaji kqtika usimamizi wa fedha.
Kupitia tuzo kama hizi, NHC linaonyesha dhamira yake ya kuboresha huduma zake na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mashirika ya umma, sekta binafsi, na wadau wa sekta ya fedha.