DODOMA-Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaendelea na maandalizi ya Siku ya Takwimu Afrika ambayo huadhimishwa tarehe 18 Novemba ya kila mwaka.
Tangu mwaka 2018, NBS imekuwa ikiandaa Shindano la Waandishi Mahiri wa Habari za Kitakwimu kila mwaka.
Shindano hili lina lengo la kuhimiza na kuchagiza matumizi ya Takwimu katika habari ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu takwimu na matumizi yake.
Kufanya hivyo, kutasaidia kujenga jamii yenye uelewa mzuri wa Takwimu na matumizi yake ili kusaidia katika kufanya maamuzi.
Hivyo basi, NBS inawaalika Waandishi wa Habari kuwasilisha kazi zaozilizochapishwa kuanzia tarehe 20 Novemba, 2023 hadi Novemba 8, 2024 zenye maudhui yanayoendana na kauli mbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa Mwaka 2024 ili ziweze kushindanishwa na kupata Waandishi Mahiri watatu kwa mwaka 2024.
Kauli mbiu ya Mwaka 2024 ni "Wezesha utoaji wa elimu kwa kuboresha uzalishaji wa Takwimu zinazokidhi malengo" Shindano hili ni kwa Waandishi walioajiriwa au wa kujitegemea wanaofanyakazi na Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makala/habari zitakazopokelewa kwa ajili ya shindano hili ni zile zilizochapishwa magazetini, kwenye mitandao ya kijamii inayochapisha habari, makala/vipindi maalumu zilizorushwa redioni katika kipindi kilichotajwa.