NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema,katika mwaka wa fedha 2023/2024 imeokoa jumla ya shilingi bilioni 14.94 kupitia ukaguzi na shilingi trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba ameyasema hayo leo Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo ya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
PPRA ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha pia inasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Msajili wa Hazina kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina Na. 370 na marekebisho yake na sheria zingine zinazoongoza Ofisi ya Msajili wa Hazina, ana mamlaka ya kusimamia shughuli zote, rasilimali zote za mashirika ya umma,
Taasisi na wakala wa Serikali, kupitia matumizi ya pesa katika mashirika ya umma na yaliyoundwa kisheria kwa lengo la kupendekeza hatua zinazolenga kuunganisha, kuvunja au kuboresha utendaji wake.
Katika hatua nyingine, Simba amesema hadi kufika Oktoba 31, 2024 jumla ya taasisi nunuzi 21,851 zimesajiliwa na zinatumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
Pia,bajeti ya ununuzi ya zaidi ya shilingi trilioni 38.6 imewekwa kwenye Mfumo wa NeST, kama fursa ya wazi kwa ajili ya wazabuni.
Vilevile, Simba amesema wazabuni zaidi ya 28,590 wamejisajili kwenye Mfumo wa NeST huku mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 10.2 imetolewa kwa wazabuni kupitia Mfumo wa NeST.
"Na ununuzi wa umma ni shughuli muhimu ya kiuchumi inayohusisha sehemu kubwa ya Pato la Taifa (GDP) takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali na taasisi zake hutumika kwenye ununuzi wa umma, hivyo ununuzi wa umma nchini unasimamiwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410."
Amesema, sheria hiyo imeunda Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo.
"Chini ya sheria hii zimeundwa Kanuni za Ununuzi wa Umma, 2024 na Miongozo kwa ajili ya kuweka taratibu za ununuzi wa umma. Kanuni mpya za Ununuzi wa Umma zimekwishakamilika."
Simba ameongeza kuwa, pia mamlaka hiyo imewezesha ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi kwa kuanzisha kanda sita katika mikoa ya Mwanza, Dar es Saalam, Arusha, Mbeya,Tabora na Mtwara.
"Na tumekamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya PPRA na kuhamia rasmi tangu mwezi Machi 2024 na hivyo kuokoa pesa ambayo ingetolewa kama kodi ya pango.
Amesema, katika kuwaongezea nguvu wazabuni wa ndani, sheria mpya ya ununuzi wa umma imeweka fursa ya wazabuni wa ndani kushirikiana na wazabuni wa nje (partnership), na katika ushiriki huo, kampuni ya ndani ndiyo itakayokuwa kampuni kiongozi na fedha zitalipwa kwa kampuni hiyo ya ndani.
"Zabuni zenye thamani isiyozidi shilingi bilioni 50 zimetengwa kwa ajili ya wazabuni wa ndani ya nchipekee.Mfumo wa NeST unaisaidia PPRA katika kulisimamia hilo kwa ufanisi zaidi."
Amesema,Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410, inazitaka taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenyeulemavu ambapo Mfumo wa NeST kama nyenzo, umesaidia utekelezaji wake.
Simba amesema kuwa, tangu mfumo wa NeST ulipoanza kutumika Julai 1, 2023 hadi Oktoba 8, 2024, jumla ya vikundi 210 (makundi maalum( vilifanikiwa kupata tuzo za zabuni zenye jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 9.855.
"Katika mwaka wa fedha uliopita, yaani tangu Julai 1, 2023 hadi Juni 30,2024 kwa ujumla, vikundi 85 vya vijana vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu na milioni mia tisa."
Simba amesema,katika makundi mengine, tangu Julai 1, 2023 hadi Juni 30,2024 vikundi 84 vya wanawake vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4 na vikundi viwili vya wazee vilipata zabuni zenye thamani ya shilingi milioni 74.