Rais Dkt.Mwinyi akutana na kampuni za uwekezaji China

SHANGHAI-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameendelea na ziara yake jijini Shanghai, China leo na kukutana na ujumbe ulioongozwa na Bw. Bai Yin Zhan kutoka kampuni ya China Harbour Engineering Co. Ltd, waliofika katika jengo la Ling Hang Group.
Kampuni hiyo, ina uzoefu wa kujenga miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa bandari, upanuzi, na uboreshaji wa miundombinu kwa viwango vya kimataifa.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mchakato wa kuipa dhamana kampuni hiyo ya China Harbour Engineering Co. Ltd kujenga Bandari ya Mangapwani, Unguja.
Katika mkutano huo, Rais Dkt. Mwinyi amemhakikishia Bw. Bai Yin Zhan kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, baada ya kukamilisha mchakato wa maridhiano kwa pande zote mbili, SMZ itatoa ushirikiano ili ujenzi wa mradi huo uanze mara moja.
Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi amekutana na wawakilishi wa kampuni mbalimbali ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza Zanzibar, zikiwemo Fuhai Group, inayojihusisha na masuala ya nishati, mafuta, na gesi; Chery Holding Group Co. Ltd, iliyobobea katika utengenezaji wa magari yanayotumia nishati ya umeme; na China Sinopharm International, kampuni kubwa inayotengeneza madawa ya binadamu.
Mazungumzo hayo yalilenga kuweka misingi ya ushirikiano itakayosaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi kupitia uwekezaji endelevu.


📅 06 Novemba 2024

📍Shanghai, China

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news