Rais Dkt.Mwinyi ashiriki maziko ya mwanahabari Biubwa Said Mbarak

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaongoza wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), familia na waumini wengine wa dini ya Kiislam kwenye maziko ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa shirika hilo, marehemu Biubwa Said Mbarak aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati akitibiwa.
Maziko hayo yamefanyika nyumbani kwa marehemu Kwaalamsha Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi na baadae Alhajj Dkt.Mwinyi alihudhuria sala ya maiti iliyohudhuriwa pia na wananchi mbalimbali.

Marehemu Biubwa kitaaluma alikuwa mwandishi wa habari alipata mafunzo ya kada hiyo kwenye Chuo cha Idara ya Habari Maelezo wakati huo mwaka 1999 na aliajiriwa na ZBC mwaka 2007.

Awali alikuwa mwandishi wa habari za Mawio, kipindi maarufu kinachorushwa kila siku asubuhi na ZBC, redio akiwa miongoni mwa watangazaji wa mwanzo wa kipindi hicho tokea kilipoanzishwa mwaka 2000.
Baadhi ya waandishi wa habari waandamizi na wafanyakazi wa ZBC, wameelezea namna walivyomfahamu marehemu Biubwa katika kazi zao, kwamba alikua mchapakazi, mweledi na mwenye ushirikiano mzuri na wenziwe na kwamba ameacha pengo kwenye tasnia ya habari.

Marehemu Biubwa alizaliwa mwaka 1972 na amezikwa kijijini kwao Jumbi, Mkoa wa Kusini Unguja.Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema,Amin.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news