Rais Dkt.Mwinyi azima zote awasha kijani huku akisisitiza kasi ya kuifungua Pemba kiuchumi

ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali inaendeleza juhudi za kuifungua Pemba kimaendeleo.

Amesema Serikali inaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kuu na za vijijini, kutengeneza bandari za Mkoani, Shumba na kuanza matayarisho ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 2, 2024 katika viwanja vya Gombani, Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipozindua Kampeni ya Kijana Kijani kwa upande wa Pemba ikiwa ni shamrashamra za kupongeza miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, anayoiongoza.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa, Serikali hadi kufikia mwezi Machi 2024, kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 31.8 kwa wajasiriamali wadogo wadogo Unguja na Pemba, ambapo asilimia 40 ya wanufaika ni vijana wa umri wa miaka 18-35.
Vilevile Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha eneo la uwekezaji la Micheweni na eneo la viwanda Chamanangwe kwa kuyawekea miundombinu, na kuongeza kuwa tayari kuna wawekezaji waliojitokeza kuwekeza katika maeneo hayo, hatua aliyoieleza kwamba itaongeza fursa za ajira kwa vijana.
Kampeni ya “Kijana Kijani” yenye kauli mbiu "Tunazima zote, tunawasha kijani" imefanikiwa kuingiza wanachama wapya 1,135 kutoka chama cha upinzani cha ACT Wazalendo na CUF, wakiwemo wanachama mashuhuri na viongozi waandamizi wa vyama hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news