Rais Dkt.Mwinyi kuzindua Ofisi na Maabara za Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia Zanzibar

DODOMA-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Husein Ali Mwinyi anatarajiwa kuzindua Ofisi na Maabara za Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia Zanzibar.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo Novemba 7,2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanahabari.

Amesema,usinduzi huo utafanyika Novemba 11,2024 huko Dunga Zuze jijini Zanzibar ikiwa ni miundombinu ya kisasa ambayo inaendandana na azma ya Rais wa Jamhuri ya Muumgano wa Tanzania, Dkt.Samia Saluhu Hassan ya kutaka huduma hiyo ipelekwe karibu na wananchi.

"Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na Tume ya Nguvu za atomu Tanzania kwa lengo la kufikisha huduma kwa wananchi wamejenga ofisi na maabara za nyuklia katika kanda nne ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha),
"Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza) na hivi karibuni tunaenda kuzindua Ofisi ya Zanzibar. Lengo la kujenga ofisi tajwa ni kusogeza huduma kwa wananchi kupitia ofisi mbalimbali za TAEC zilizopo katika kanda husika."

Amesema,hatua hiyo ni sehemu yautekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, ilielekezwa kuhakikisha inaendelea kuimarisha huduma, tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza wigo wa matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali nchini.

"Sambamba na hilo, hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za uthibiti na kuhamasisha matumizi salama ya nyuklia karibu na wananchi wa Zanzibar."

Waziri Prof.Mkenda amesema,teknolojia ya nyuklia ikitumika vizuri inaweza kuongeza tija katika sekta mbalimbali.
"Mathalani, teknolojia hii inatumika kuchunguza na kutibu ugonjwa wa saratani, kuboresha mbegu za mazao hasa yale ambayo yana ugumu kustawi na yanatoa mazao kidogo."

Pia, amesema inasaidia kuua vimelea vinavyosabisha chakula kuharibika, kudhibiti kuzaliana kwa wadudu wanaoeneza magonjwa kama vile mbung'o, kuhakiki uimara na ubora wa maungio ya matenki na mabomba makubwa ya mafuta au maji.

Vilevile, kuhakiki ubora katika ujenzi wa barabara na reli, kusafisha maji taka kwa ajili ya kutumika katika shughuli nyingine (recycling) utafiti wa mafuta na gesi na kadhalika.

"Pamoja na manufaa yaliyoainishwa, katika nchi yetu kumekuwa na ongezeko kubwa la fursa za kutumia Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, afya, viwanda,mifugo, na maji."

Amesema,matumizi ya teknolojia hii yatachangia maendeleo katika nyanja hizo kwa kuboresha uzalishaji,kuongeza ubora wa bidhaa, na kuhakikisha usalama na ufanisiwa huduma zinazotolewa.
"Hata hivyo, ili fursa hizi zitumike kikamilifu na kwa ufanisi, kuna haja ya kuwa na miundombinu ya kisasa na madhubuti ambayo itawawezesha wataalamu wetu na wanasayansi kufanya kazi katika mazingirabyanayowezesha ubunifu na ugunduzi mpya."

"Kwa muktadha huo, uwepo wa maabara mpya upande wa Zanzibar ni hatua muhimu sana katika kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia yanakua na kuleta tija inayokusudiwa.

"Maabara hizi zitakuwa msingi mzuri wa shughuli za utafiti na mafunzo, zikiwawezesha wataalamu wetu kufanikisha tafiti na miradi mbalimbali inayolenga kuboresha huduma na bidhaa katika sekta hizo muhimu."

Waziri Mkenda amesema,matumizi ya maabara hizi pia yatasaidia kuongeza fursa za kufanya biashara na nchi nyingine kwa kuhakikisha usalama wa bidhaa zinazoingia na kutoka nje ya nchi yetu.
Aidha, amesema uwepo wa maabara hii utaongeza uwezo wa kitaaluma wa wataalamu wetu, kuwezesha uhamishaji wa teknolojia, na
kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia.

"Mtakumbuka kwamba,kutokana na manufaa makubwa ya teknolojia ya nyuklia,Serikali ilizindua ufadhili kupitia skolashipu ya 'SamiaExtended' inayolenga kusomesha vijana wa Kitanzania nje ya nchi katika ngazi ya Umahiri kwenye masuala ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia."
Waziri Mkenda amesema,kuanzia mwaka huu, vijana watano wa Kitanzania watapata ufadhili wa shahada hizo za umahiri.

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau, amesema itaendelea kuongeza kiwango cha ufadhili kulingana na uwezo wa kibajeti ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na wataalamu wa kutosha kati nyanja husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news