Rais Dkt.Samia amteua Mheshimiwa Chande kuwa Kiongozi wa SADC-SEOM nchini Mauritius

PORT LOUIS-Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemteua Mheshimiwa Mohammed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, kuwa Kiongozi wa Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC - SEOM) katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Mauritius unaotarajiwa kufanyika tarehe 10 Novemba, 2024.
Mheshimiwa Chande ambaye amewasili Mjini Port Louis, Jamhuri ya Mauritius Jumatatu, tarehe 4 Novemba 2024, anatarajiwa kuzindua rasmi Misheni hiyo mapema tarehe 5 Novemba, ambayo inawaangalizi wa uchaguzi takriban sabini kutoka nchi tisa wanachama wa jumuiya hiyo kongwe barani Afrika.

Waangalizi hao wa uchaguzi wanaotarajiwa kuanza kazi baada ya kupitia mafunzo maalum ya siku nne ya uangalizi wa uchaguzi, watapelekwa kwenye wilaya zote kumi za kiutawala nchi nzima, ikiwemo Kisiwa cha Rodrigues.
Mhe. Chande ambaye ameambatana na wajumbe mbalimbali kutoka Tanzania akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe. Jaji Francis Mutungi, ataungana na wajumbe wa nchi mbili ambao wapo kwenye uongozi wa utatu wa asasi hiyo yaani Troika (Zambia na Malawi) na kufanya mikutano na wadau mbalimbali wa uchaguzi nchini Mauritius ikiwemo Vyama vya Siasa,

Tume ya Uchaguzi, Wizara ya Mambo ya Nje, Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo, Jumuiya za Kimataifa, Asasi za Kiraia, Taasisi za Dini na Vyombo vya Habari kwa ajili ya kuelezea kazi ambayo SEOM itafanya kama muangalizi wa uchaguzi.
Viongozi wengine wa Kitaifa ambao hivi karibuni wameteuliwa na Rais Dkt. Samia kama viongozi wa misheni za uangalizi wa chaguzi za Msumbiji na Botswana ni Mhe. Abeid Amani Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mstaafu, pamoja na Mhe. Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news