BRAZIL-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuongoza timu ya kukagua majengo yote ya Kariakoo ili kupata taarifa kamili ya hali ya majengo baada ya kumaliza zoezi la uokoaji.
Akizugumza na watanzania kupitia vyombo vya habari Novemba 17, 2024 kuhusu tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amesema kuwa,baada ya zoezi la uokozi kukamilika Waziri Mkuu ataongoza timu ya wakaguzi wa majengo katika soko hilo.
Pia, amesema kuwa Serikali itaweka wazi kuhusu taarifa ya uchunguzi baada ya kupatikana pamoja na kuchukua hatua.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo."
Rais Dkt.Samia amesema,kufuatia tukio hilo amepata taarifa za mara kwa mara kutoka kwa Waziri Mkuu kuhusu mwenendo wa uokoaji unavyoendelea.