NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa ndugu, jamaa,watumishi na marafiki kutokana na kifo cha Bw. Lawrence Nyasebwa Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyabainisha hayo leo Novemba 9,2024 kupitia taarifa aliyochapisha katika mitandao yake ya kijamii.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Bw. Lawrence Nyasebwa Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kilichotokea leo tarehe 09 Novemba, 2024 katika hospitali ya Apollo nchini India.
"Ninatoa pole kwa familia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Mheshimiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo, watumishi wa Tume ya Mipango, ndugu jamaa na marafiki kufuatia msiba huu.
"Bw. Mafuru atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka, bidii na ubunifu alipotumikia nafasi mbalimbali ndani ya Serikali.
"Mwenyezi Mungu aijalie familia yake subra na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na ailaze roho yake mahali pema.Amina,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.