NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa za ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika Kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Aidha,Rais Dkt.Samia ametoa maelekezo kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuhakikisha kazi ya uokoaji inafanyika kwa haraka.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Novemba 16,2024 kupitia kurasa zake rasmi za kijamii huku akitaka kupewa taarifa za kila mara kuhusu kinachoendelea.
"Nimesikitika kupokea taarifa ya ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.
"Nimeuagiza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi.
"Wakati hilo likiendelea na tukimuomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi, tuwaombee pia utulivu na subra ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii.
"Hivi punde nimezungumza kwa kirefu na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge) kuhusiana na ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na kazi ya uokoaji inayoendelea.
"Nimempa maelekezo kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa haraka na ufanisi, na niendelee kupata taarifa ya kila hatua ya maendeleo yake," amesisitiza Rais Dkt.Samia.